MALI-SIASA-USALAMA

Kiongozi wa mapinduzi nchini Mali aitaka ECOWAS kuondoa vikwazo dhidi ya nchi yake

Kiongozi wa mapinduzi nchini Mali,, Assimi Goïta, wakati wa sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya uhuru wa Mali, huko Bamako, Septemba 22, 2020.
Kiongozi wa mapinduzi nchini Mali,, Assimi Goïta, wakati wa sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya uhuru wa Mali, huko Bamako, Septemba 22, 2020. MICHELE CATTANI / AFP

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali Kanali Assimi Goita, anataka mataifa ya Afrika Magharibi chini ya Jumuiya ya Kiuchumi ya ECOWAS kuiondolea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi ambavyo amesema vinatishia uchumi wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kanali Goita amesema baada ya jeshi kumteua Bah Ndaw kuwa rais wa mpito, vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa haraka iwezekanavyo, kauli aliyoitoa wakati nchi hiyo ikidhimisha miaka 60 ya uhuru siku ya Jumanne.

Kauli hii imeungwa mkono na kiongozi wa upinzani Abdoulaye keita.

Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewataka viongozi wa kijeshi kukabidhi madaraka yote kwa kiongozi wa kiraia na kuonya kuwa ushirikiano wa nchi yake katika vita dhidi ya ugaidi nchini humo, utategemea hatua hiyo.

Mapema wiki hii uongozi wa kijeshi nchini Mali, uliwataja viongozi wa serikali ya mpito, hatua inayokuja kufuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, na Jumuiya ya Kimataifa, kutaka jeshi kukabidhi madaraka kwa raia.

Hatua hii imekuja baada ya mkutano wa wiki iliyopita kati ya wanajeshi nchini Mali na viongozi wa ECOWAS ambao wameiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi ya Mali, kama njia mojawapo ya kuharakisha uteuzi wa raia kuongoza serikali hiyo.

Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa uteuzi wa Bah N'Daw, mwenye umri wa miaka 70 na mwanajeshi wa zamani, ni ishara kuwa jeshi nchini humo hawataki kuachia madaraka moja kwa moja baada ya kusema kuwa wanataka kuongoza serikali hiyo ya mpito.

Rais huyo wa mpito alihudumu kama Waziri wa Uinzi chini ya rais wa zamani Ibrahim Boubakar Keita aliyeondolewa madarakani mwezi Agosti na anatarajiwa kuongoza kwa muda wa miezi kumi na minane kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

Uteuzi wake umezua maoni mbalilbali katika taifa hilo la Afrika Magharibi kutoana na uhusiano wake na wanajeshi.