DRC-USALAMA

Ituri: Watu 1,800 wauawa na 1,600,000 wayatoroka makazi kwa kipindi cha miezi 6

Jeshi la DRC, FARDC,  linaendelea na mashambulizi dhidi ya kundi la wanamgambo la FRPI katika mkoa wa Ituri.
Jeshi la DRC, FARDC, linaendelea na mashambulizi dhidi ya kundi la wanamgambo la FRPI katika mkoa wa Ituri. Photo MONUSCO/Abel Kavanagh

Katika kipindi cha miezi sita, katika mkoa wa Ituri, zaidi ya watu 1,800 wameuawa, 1,600,000 wameyatoroka makazi yao, shule 300 zimeharibiwa katika mkoa wa Ituri, kulingana na Radio ya Umoja wa Mataifa nchini DRC, OKAPI, ikimnukuu mbunge Jackson Ausse.

Matangazo ya kibiashara

Idadi hii imewekwa wazi na mbunge wa kitaifa Jackson Ausse, katika barua ya wazi iliyotumwa Jumanne, Septemba 22 kwa Rais Felix Antoine Tshisekedi.

Katika barua hii, mbunge Jackson Ausse amezungumzia kuongezeka kwa athari za kibinadamu zinazosababishwa na ukosefu wa usalama katika mkoa wa Ituri tangu mwezi Machi mwaka huu.

Katika kukabiliana na hali hii ya usalama na hali ya kibinadamu, mbunge Jackson Ausse amemuomba rais Felix Tshisekedi kutangaza hali ya dharura ya usalama katika katika mkoa wa Ituri hili na vile vile katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Hayo yanajiri wakati mapigano ya kikabila katika mkoa wa Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yamesababisha vifo vya watu 11 na wengine zaidi ya Elfu 10 kuyakimbia makwao huku nyumba zaidi ya Elfu moja yakiteketezwa moto, katika mapigano hayo yaliyotokea mapema mwezi huu.

Ripoti ya Shirika lisilokuwa la kiserikali la kanisa katoliki CARITAS,limesema mapigano hayo yalianza tarehe tano Septemba na kuendelea kwa siku tatu mfululizo.Chanzo cha machafuko hayo, yaliyohusisha watu kutoka jamii ya Bena Kabuya, Bena Mwembia na Bena Nshimba ni mgogoro kuhusu umiliki wa ardhi Mkuu wa shirika hilo Pierre Mulumba amesema kufikia sasa watu 11 wamepoteza maisha ,wengine elfu kumi wakiliazimika kukimbia makwao ,na nyumba karibu elfu moja zikiwa zimechomwa moto.Shirika hilo la Kanisa Katoliki linatarajiwa kuzuru eneo hilo, kujionea hali ilivyo baada ya mapigano hayo ambayo pia yaliwahi kuzuka kati ya ya mwaka 2016 na 2017 na kusababisha maafa.

Mkoa wa Kasai umeendelea kushuhudia ukosefu wa usalama kwa karibu miaka miwili sasa baada ya maafisa usalama kumuua Kamuina Nsapu kiongozi mkubwa wa kijamii.

Tangu Septemba mwaka 2016 na mwezi Oktoba mwaka 2017 watu zaidi ya Elfu tatu walipoteza maisha katika eneo hilo, huku wengine zaidi ya Milioni 1 na Laki Nne wakiyakimbia makwao.