MALI-SIASA-USALAMA

Bah N'Daw aapishwa kuwa rais wa mpito nchini Mali

Rais wa mpito wa Mali, Bah N'Daw, wakati wa hafla ya kuapishwa kwake huko Bamako Septemba 25, 2020.
Rais wa mpito wa Mali, Bah N'Daw, wakati wa hafla ya kuapishwa kwake huko Bamako Septemba 25, 2020. Michele Cattani / AFP

Nchini Mali, Waziri wa zamani wa Ulinzi Bah N'Daw, ameapishwa leo Ijumaa jijini Bamako kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo kwa muda wa miezi 18 ijayo, baada ya kuteuliwa na viongozi wa jeshi mapema wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Afisa mstaafu wa jeshi la Mali na rais wa mpito Bah N’Daw, pamoja na makamu mpya wa rais, Kanali Assimi Goïta, wameapishwa leo Ijumaa, Septemba 25.

Sherehe hizi zimefanyika katika hali ya kipekee, mwezi mmoja zaidi baada ya mapinduzi ya kijeshi na wakati ECOWAS bado haijaondoa vikwazo ambavyo vinaikabili nchi hiyo.

Sherehe zilicheleweshwa baaada ya kusubiri rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo ambaye ujio wake kwenye sherehe hizo ulikuwa wa kushtukiza. Ni rais pekee wa kigeni aliyehudhuria sherehe hizo wakati Mali bado iko chini ya vikwazo vya majirani zake.

Msuluhishi wa mzozo wa Mali kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Goodluck Jonathan, rais wa zamani wa Nigeria, pia amehudhuria kwenye sherehe hizo.

N'Daw, mwenye umri wa miaka 70, alionekana kwa mara ya kwanza hadharani siku ya Alhamisi, alipokutana na msuluhishi huyo wa ECOWAS wakati wa mazungumzo ya ana kwa ana.

Uteuzi wake ulitangazwa siku ya Jumatatu na Kanali Assmi Goita, ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo baada ya kuondolewa madarakani kwa rais wa zamani Ibrahim Boubakar Keita.

Kanali Goita, naye atahudumu kama Makamu wa rais.

Baada ya sherehe za leo, serikali itakayoongozwa na Waziri Mkuu ambaye atakuwa raia inatarajiwa kutangazwa na baadaye kuundwa kwa Baraza la Mawaziri.

Wakuu wa nchi za ECOWAS wanatarajiwa kuiondolea Mali vikwazo vya kiuchumi baada ya sherehe za leo.