NIGERIA-USALAMA

Kumi na Tano waangamia katika shambulio la wanajihadi Nigeria

Jimbo la Borno, limeendelea kukumbwa na mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu.
Jimbo la Borno, limeendelea kukumbwa na mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu. RFI/Moïse Gomis

Waasi wa kijihadi wenye mafungamano na kundi la Islamic State Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wamewauwa katika shambulizi la kushtukiza maafisa 15 wa kikosi cha ulinzi cha gavana wa Jimbo la Borno, ambaye amenusurika, vyanzo vya usalama vimesema.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na vyanzo hivyo, maafisa wanane wa polisi, askari watatu na watu wane kutoka kundi la wanamgambo linalounga mkono serikali waliuawa katika shambulio dhidi ya msafara wa magari ya gavana wa Jimbo la Borno, Babagana Umara Zulum, karibu na mji wa Baga kwenye mwambao wa Ziwa Chad.

Washambuliaji walishambulia msafara huo kwa bunduki za rashasha na silaha za kivita wakati msafara huo ulikuwa ukipita katika kijiji kilicho karibu na makao makuu ya Kikosi cha Pamoja cha Kimataifa (MNJTF), kinachoundwa na askari kutoka Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.

"Gavana yuko salama na mzima, lakini maafisa 15 wa kikosi chake cha ulinzi wameuawa katika mapigano na magaidi," kilisema chanzo kimoja.

Gavana huyo alikuwa amezuru Baga kama sehemu ya maandalizi ya kurudi kwa maelfu ya wakazi waliofukuzwa katika mji huo na wanajihadi mwaka 2014, kulingana na chanzo hiki. Aliondolewa eneo hilo na helikopta kwenda katika mji wa Monguno, kilomita 60 na eneo la tukio, na kurudi Baga kwa gari akisindikizwa na magar ya kijeshi chini ya ulinzi mkali, chanzo kingine kimesema.