DRC-WHO-UN-HAKI

Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada washtumiwa kuwanyanyasa wanawake DRC

Vitengo vya utunzaji wa dharura katika kituo cha matibabu cha Ebola cha shirika la matibabu ya kibinadamu Alima, huko Beni, mashariki mwa DRC.
Vitengo vya utunzaji wa dharura katika kituo cha matibabu cha Ebola cha shirika la matibabu ya kibinadamu Alima, huko Beni, mashariki mwa DRC. REUTERS/Baz Ratner

Wanawake zaidi ya 50 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanawashtumu wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali kwa unyanyasaji wa kijinsia.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Afya Duniani, WHO, ambalo ni mojawapo ya mashirika hayo yanayonyooshewa kidole, limesema kuwa limeanziisha uchunguzi.

Hayo yamo katika uchunguzi wa mashirika ya The New Humanitarian na Thomson Reuters Foundation.

Matukio hayo yalitokea kati ya mwaka 2018 na 2020 wakati wa mapambano dhidi ya virusi vya Ebola. Wanawake, ambao hawakuwahi kuripoti visa hivyo vya ubakaji kwa kuhofia ulipizaji kisasi, wanawashutumu wafanyakazi kadhaa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa namashirika yasiyo ya kiserikali kuwanyanyasa kijinsia.

Wanawake hao walikuwa wapishi, na wengine walikuwa wakijihusisha na kazi mbalimbali ya usafi katika ofisi za mashirika hayo, na walikuwa wakilipwa kati ya Dola 50 na Dola 100 kwa mwezi. Jumla ya wanawake 51 wanashutumu wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa kuwanyanyasa kijinsia. Kati yao, angalau 30 wanasema kwamba wafanyakazi wa Shirika la Afya Duniani walihusika.

WHO, ambayo ilisema Jumanne kwamba wafanyakazi wake "wamebebeshwa kashfa kubwa" kutokana na madai hayo, imeanzisha uchunguzi wa ndani.

“Vitendo vinavyodaiwa kufanywa na watu wanaodai kufanya kazi kwa WHO havikubaliki na vitachunguzwa kikamilifu. (...) Mtu yeyote ambaye atakutikana na hatia hiyo atakabiliwa na adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi mara moja, ”ilisema taarifa ya WHO.