SUDAN-MKATABA-USALAMA-SIASA

Serikali ya Sudan kutia saini mkataba wa amani na waasi

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok wakati wa ziara yake jijini Darfur Novemba 4, 2019.
Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok wakati wa ziara yake jijini Darfur Novemba 4, 2019. ASHRAF SHAZLY / AFP

Serikali ya Sudan na waasi, Jumamosi Oktoba 3, watatia saini mkataba wa amani jijini Juba katika nchii jirani ya Sudan Kusini, unaonuiwa kumaliza mapigano ya muda mrefu ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Matangazo ya kibiashara

Pande zote mbili zinatarajiwa kusaini mkataba huo mjini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, ambayo imetoa mchango mkubwa wa ushauri kwa makundi ya waasi kuweka silaha chini kwa minajili ya kurejesha amani baada ya mapigano ya zaidi ya miaka thelathini.

Kusainiwa kwa mkataba huo kunakuja wakati ambapo nchi ya Sudan ina serikali mpya na mojawapo ya malengo yake ni kumaliza uasi nchini humo.

Kufungamana na mkataba huo, vikosi vya waasi vitajiunga kwa taratibu na jeshi la serikali ya Sudan.

Ingawaje makundi tisa ya waasi yatasaini mkataba huo wa amani, kuna makundi mawili ambayo kufikia sasa yamekataa kusaini mkataba huo. Kundi moja ni Sudan Liberation Movement, la waasi lenye makao yake katika jimbo la Darfur na ambalo linaongozwa na Abdelwahid Nour.

Kundi la pili la Sudan Peoples Liberation Movement-North, lina makao yake katika jimbo la Korodofan-Kusini na linaongozwa na Abdelaziz Hilu.