Mali: Wanajihadi zaidi ya mia moja na wafungwa waachiliwa huru
Imechapishwa:
Mamlaka nchini Mali imewaachilia huru wanajihadi zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na wafungwa waliokuwa wamehukumiwa. Zoezi ambalo linaweza kuwezesha kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na wanajihadi katika kanda la Sahel.
Wanajihadi hawa walikuwa walikamatwa wakati wa operesheni kadhaa za kijeshi.
Kulingana na duru za kuaminika, zoezi hilo la kuachiliwa huru wanajihadi na wafungwa hao lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika maeneo mawili. Kuelekea katikati, na hasa Kaskazini mwa nchi. Vyanzo kadhaa vimebaini kwamba angalau wafungwa wengine wa kijihadi walioachiliwa huru tayari wamesafirishwa kwa ndege kwenda Tessalit, katika eneo linalopakana na Algeria.
Kulingana na mashuhuda baada ya kuwasili Tessalit, waliingia kwenye magari na kuelekea kaskazini mwa jiji, kabla ya kutoweka msituni. Kulingana na vyanzo vyetu, miongoni mwa wanajihadi walioachiliwa huru na Mali, na pengine pia na nchi nyingine jirani, kuna watu ambao walihusika katika mashambulio yaliyotekelezwa katika kanda hiyo.
Kuhusu sababu ya kuachiliwa kwa wanajihadi hao, duru za kuaminika, zinabaini kwamba, zoezi hilo linaendana na sehemu ya mazungumzo, mazungumzo ili kuweza kuachuliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na awanajihadi. Miongoni mwa mateka wanaoshukiwa kuwa wanaweza kuachiliwa kutokana na zoezi hilo, ni pamoja na Soumaïla Cissé, kiongozi wa upinzani katika bunge lililovunjwa nchini Mali, ambaye alitekwa mwezi Machi Kaskazini mwa nchi na watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi. Na mwengine ni Sophie Pétronin, raia wa Ufaransa, ambaye alitekwa nyara mwezi Desemba 2016 Kaskazini mwa Mali.