DRC-UN-USALAMA

UN yachukizwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia DRC

Shirika la afya duniani WHO limesema linachunguza madai ya vitendo vya unyanyasaji wa kimapenzi vilivyofanywa na wafanyakazi wake dhidi ya wanawake zaidi ya 50, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati wa kukabiliana na janga la Ebola, kati ya mwaka 2018 hadi 2020.

Moja ya maeneo ya mji wa Butembo, Kivu Kaskazini, kitovu cha mlipuko wa virusi vya Ebola, mashariki mwa DRC.
Moja ya maeneo ya mji wa Butembo, Kivu Kaskazini, kitovu cha mlipuko wa virusi vya Ebola, mashariki mwa DRC. JOHN WESSELS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Katika mahojiano maalum na RFI Kiswahili, baadhi ya wanawake hao wamesema walifanyiwa vitendo hivyo na wanaume waliosema ni wafanyakazi wa WHO, ili wapate kazi.

Hivi karibuni uchunguzi wa mashirika ya The New Humanitarian na Thomson Reuters Foundation ulibaini kwamba matukio hayo yalitokea kati ya mwaka 2018 na 2020 wakati wa mapambano dhidi ya virusi vya Ebola. Wanawake, ambao hawakuwahi kuripoti visa hivyo vya ubakaji kwa kuhofia ulipizaji kisasi, wanawashutumu wafanyakazi kadhaa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali kuwanyanyasa kijinsia.

Wanawake hao walikuwa wapishi, na wengine walikuwa wakijihusisha na shughuli mbalimbali za usafi katika ofisi za mashirika hayo, na walikuwa wakilipwa kati ya Dola 50 na Dola 100 kwa mwezi.

Jumla ya wanawake 51 wanashutumu wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa kuwanyanyasa kijinsia. Kati yao, angalau 30 walisema kwamba wafanyakazi wa Shirika la Afya Duniani walihusika.