NIGERIA-MAANDAMANO-USALAMA

Nigeria yaendelea kukumbwa na maandamano

Maandamano yameendelea kushuhudiwa nchini Nigeria, kulaani dhuhuma zinazodaiwa kufanywa na jeshi la Polisi nchini humo, licha ya serikali kuahidi, kulifanyia mageuzi na kuvunjwa kwa kikosi maalum cha SARS kilichokuwa kimepewa kazi ya kupambana na wahalifu.

Maandamano yaendelea Nigeria, kulaani dhuhuma zinazodaiwa kufanywa na jeshi la Polisi nchini humo.
Maandamano yaendelea Nigeria, kulaani dhuhuma zinazodaiwa kufanywa na jeshi la Polisi nchini humo. REUTERS/Afolabi Sotunde
Matangazo ya kibiashara

Waandamanaji siku ya Jumatano wamefunga barabara kuu jijini Lagos, huku wakionekana wenye hasira kwa kile walichokisema kuwa wamechoshwa kuhangaishwa na maafisa wa Polisi.

Licha ya serikali Jumapili iliyopita, kutangaza kufutwa kwa kikosi hicho maalum cha polisi kilichopewa kazi ya kupambana na wahalifu katika majimbo mbalimbali, waandamanaji wanasema hawajaridhika na hatua hiyo na haiwaamini serikali na wanachokitaka ni mageuzi katika jeshi hilo.

Siku ya Jumanne, Mkuu wa Jeshi la Polisi alitangaza kuanziwa kwa kikosi kipya kinachofahamika kama SWAT ambacho sasa kitakuwa na kazi ya kupokonya watu wanaomiliki silaha kinyume na sheria.

Maandamano pia yameshuhudiwa katika jiji kuu Abuja, huku serikali ikisema ina nia ya dhati ya kulifanyia mageuzi jeshi hilo, kauli ambayo imeungwa mkono na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Edward Kallon.