LIBYA-SIASA-USALAMA

Salamé: Hali haijuruhusu kupatikana kwa mkataba wa amani Libya

Mjumbe maalumu wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amezilaumu nchi zinazoendeleza siasa za unafiki nchini Libya, hali ambayo inasababisha kushindwa kupatikana kwa mkataba wa amani, Ghassan Salamé amesema.

Libya inaendelea kukumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Libya inaendelea kukumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Abdullah DOMA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Ghassan Salamé amesisitza kuwa baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama wanamuunga mkono Jenerali muasi Khalifa Haftar na kuvunja nguvu juhudi za Umoja wa Mataifa za kuutatua mgogoro wa Libya.

Katika mahojiano maalum na kituo cha France 24 Ghassan Salamé amefahamisha kuwa muda haujafika bado kwa Walibya kukubali kuungana pamoja na kuijenga nchi yao.

Hivi karibuni Uturuki iliahidi mshikamano kamili na serikali ya umoja wa kitaifa Libya, inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Vita vya Libya ni vita vya washirika. Nchi nyingi za kigeni zinahusika katika suala hili. Uturuki na Urusi ni washirika wawili kati ya pande mbili hasimu katika mzozo huo.

Nchi hizo mbili zinaunga mkono kambi mbili zinazokinzana nchini Libya. Moscow inaunga mkono mbabe wa kivita mashariki mwa Libya, Marshal Haftar, wakati Ankara ikiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao makuu jijini Tripoli, na kambi ya Magharibi mwa Libya kwa ujumla. Nchi zote mbili hizi zimetuma idadi kubwa ya silaha na maelfu ya wanajeshi nchini Libya. Wapiganaji wanaojulikana kwa jina la "Wagner" na vile vile mamluki kutoka Syria wanaounga mkono Urusi, mamluki kutoka Syria na mataifa mengine mengi kwa upande wa Uturuki wako nchini Libya kusaidia pande mbili hasimu katika vita hivyo.

Kwa hiyo, Urusi na Uturuki zinashindana nchini Libya kama vile nchini Syria. Kila nchi inatafuta kuongeza ushawishi wake, huku ikijaribu kutafuta maelewano, bila hata hivyo kufanikiwa.