DRC-USALAMA-SIASA

Suala la Minembwe DRC: Daktari Mukwege awashuhshia lawama wanasiasa

Katika hospitali ya Panzi huko Bukavu (Kivu Kusini), waathiriwa ni kutoka jamii zote.
Katika hospitali ya Panzi huko Bukavu (Kivu Kusini), waathiriwa ni kutoka jamii zote. Sonia Rolley/RFI

Licha ya uamuzi wa Rais Tshisekedi wa kusitisha zoezi la kuwekwa kwa wilaya ya Minembwe, suala hili linaendelea kusababisha mgawanyiko katika jamii mbalimbali nchini DRC.

Matangazo ya kibiashara

Wilaya hii iliyoko nyanda za juu katika mkoa wa Kivu Kusini iliundwa na sheria ya kirais ya mwaka mnamo 2013. Hapa ndipo wanaishi watu kutoka jamii ya Banyamulenge (raia wa DRC wenye asili ya Rwanda) wanaoshutumiwa na Wacongo wengine kuwa sio wananchi wa DRC, kwamba wanataka kuchukua ardhi katika maeneo mengine au hata kuigawa nchi hiyo.

Wanasiasa katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, wanaendelea kusababisha hali ya sintofahamu juu ya suala la kuwapo au la kwa wilaya ya Minembwe na matamshi ya chuki yanayoendelea kuongezeka.

Hata kama machafuko yamepungua kwenye milima ya Minembwe tangu kuzuka kwa utata huu mwishoni mwa mwezi Septemba (wakati wa zoezi la kumkabidhi madaraka meya wa wilaya hiyo, lililositishwa tangu wakati huo), Daktari Denis Mukwege ana wasiwasi juu ya yaliyomo kwenye matamshi yanayoendelea kutolewa kuhusu suala hili.

Kwa upande wa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, anasema wanasiasa huko Kinshasa, kutoka jamii zote, wanajaribu kutoa kauli za uchochezi kuhusu suala hilo wakati wakaazi wa eneo hilo ndio huteseka.

"Wanasiasa huko Kinshasa, wangeweza kushughulikia maswala haya badala ya kutumia muda wao kueneza matamshi ya chuki ambayo yanasababisha vurugu zaidi, " ameongeza Daktari Mukwege.

Amewanyooshea kidole cha lawama wanasiasa kutoka vyama vyote kushindwa kutafutia suluhu suala la Minembwe.