LIBYA-HAKI ZA BINADAMU

Visa vya utekaji nyara vyaongezeka nchini Libya

Moja ya mitaa huko Tripoli, Libya, Januari 13, 2020.
Moja ya mitaa huko Tripoli, Libya, Januari 13, 2020. Mahmud TURKIA / AFP

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Libya (NHCR) inalaani kuzuiliwa kiholela kwa mmoja wa wakurugenzi wake ambaye yuko kizuizini tangu Oktoba 1.

Matangazo ya kibiashara

Walid Elhouderi anahusika na masuala ya mawasiliano na uratibu wa kimataifa katika Tume hiyo. Alichukuliwa na vikosi chini ya amri ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj huko Tripoli.

Kuzuiliwa kwake kiholela kunaangazia tabia sugu inayoendelea nchini Libya.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Libya (NHCR) inashutumu kuzuiliwa "kimabavu na kiholela" kwa mmoja wa maafisa wake na imetoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri Mkuu na tume ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, kusaidia ili achiliwe haraka iwezekanavyo. NHCR inainyooshea kidole cha lawama serikali ya Tripoli na kusema ndo itaulizwa kuhusu usalama wake.

Tume hiyo imebaini kwambamaafisa wa idara ya ujasusi ndo walimteka nyara Walid Elhouderi, mtoto wa balozi wa sasa wa Libya nchini Ufaransa na mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye RFI imekuwa ikimhoji mara kwa mara.

NHCR inasema "inasikitishwa sana" na dhuluma zote zinazowakumba raia na wanaharakati wa haki za binadamu nchini Libya. Kama raia wengine wengi wa Libya, Walid Elhouderi alitekwa nyara bila waranti, anashikiliwa bila sababu, na hadi Oktoba 1, hajafikishwa mbele ya mwendesha mashitaka mkuu.

Pamoja na wafungwa zaidi ya 1,600 waliorekodiwa mnamo 2019, Libya inaongoza kwa orodha nyeusi ya nchi za Afrika kuwazuia watu kiholela na visa vya watu kutoweka kiholela.

Mwezi Machi, tume ya Umoja wa Mataifa huko Tripoli ilionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali hii na kuongezeka kwa vitendo vya dhulma dhidi ya raia vinavyofanywa na vikosi vya jeshi bila adhabu kuchukuliwa adhabu yoyote.