GUINEA-SIASA-USALAMA

Waguinea wasubiri matokeo ya uchaguzi wa urais

Raia wa Guinea wanaendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili Oktoba 18. Rais anayemaliza muda wake Alpha Condé, 82, anawania muhula wa tatu baada ya kupitishwa kwa katiba mpya, hali iliyozua utata kati ya wanasiasa nchini Guinea.

Waguinea wanasubiri kupiga kura katika uchaguzi wa urais, Oktoba 18, 2020, huko Fria.
Waguinea wanasubiri kupiga kura katika uchaguzi wa urais, Oktoba 18, 2020, huko Fria. REUTERS/Saliou Samb
Matangazo ya kibiashara

Kwa jumla, karibu wapiga kura milioni 5.5 wamepiga kura kumchagua rais wao mpya kati ya wagombea kumi na wawili wanaowania kiti hicho.

Baada ya miezi kadhaa ya maandamano mabaya dhidi ya muhula wa 3 wa rais Alpha Condé, wananchi wa Guinea walipiga kura kumchagua kiongozi wao mpya. Uchaguzi huo ulifanyika kwa amani, lakini pia kwa wasiwasi wa uwezekano wa kuzuka vurugu wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Hata kabla ya kuanza kwa zoezi la kukusanya matokeo ya uchaguzi, upinzani umeanza kulaani kitendo ch akujaribu kujaza kura mbele ya wawakilishi wake katika vituo vya kupigia kura, hasa huko Haute Guinea, ngome ya kijadi ya chama tawala na katika eneo la kusini.

Waziri mkuu Ibrahima Kassory Fofana amewaambia waandishi wa habari kuhusu hitilafu ndogo zilizojitokeza hapa na pale, na hakuweza kutoa maelezo zaidi.