GUNIEA-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Guinea: Dalein Diallo ajitangaza mshindi wa uchaguzi, CENI yamuonya

Wakati zoezi la uhesabuji kura likiendelea nchini Guinea, kiongozi wa chama cha upinzani cha Union of Democratic Forces of Guinea (UFDG) Cellou Dalein Diallo amejitangaza kuwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu huo ambao ulifanyika siku ya Jumapili iliyopita

Makabiliano yazuka karibu na makaazi ya kiongozi wa upinzani Cellou Dalein Diallo ambaye anadai kushinda uchaguzi wa urais, Jumatatu Oktoba 19, 2020.
Makabiliano yazuka karibu na makaazi ya kiongozi wa upinzani Cellou Dalein Diallo ambaye anadai kushinda uchaguzi wa urais, Jumatatu Oktoba 19, 2020. RFI/Carol Valade
Matangazo ya kibiashara

Diallo amewataka wafuasi wake kuwa waangalifu zaidi katika kuutetea ushindi wake huo alioutaja kuwa ni wa kidemokrasia.

Diallo hakutoa takwimu zozote lakini alisema matokeo hayo ni kwa mujibu wa chama chake, na sio hesabu rasmi ya tume ya kitaifa ya uchaguzi, ambayo bado haijachapisha matokeo.

Kufuatia kauli yake hiyo, wafuasi wake walitawanyika barabarani kushangilia ushindi. Diallo amesema kwamba vijana watatu waliuawa katika mji mkuu wa Conakry, na wengine kadhaa walijeruhiwa na vikosi vya usalama wakati walisherehekea ushindi wake.

Kwa upande wake Tume huru ya uchaguzi, CENI, imesema kuwa kiongozi huyo wa upinzani atakabiliwa na adhabu kali kwa kukiuka sheria za uchaguzi.

Ni Uchaguzi ambao ulikuwa na wagombea 12 lakini washindani wakuu ni rais wa sasa Alpha Conde, mwenye umri wa miaka 82 na kiongozi wa upinzani Cellou Dalein Diallo.