COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA

Uchaguzi wa urais Cote d'Ivoire: Hali ya wasiwasi yatanda Dabou

Vikosi vya usalama vilitumwa kurejesha utulivu Dabou.
Vikosi vya usalama vilitumwa kurejesha utulivu Dabou. ISSOUF SANOGO / AFP

Ikiwa zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi wa urais nchini Cote d'Ivoire, mji wa Dabou, magharibi mwa Abidjan, katika siku mbili zilizopita ulipitia moja ya vipindi vigumu zaidi tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga Alassane Ouattara kuwania muhula wa tatu.

Matangazo ya kibiashara

Machafuko ya hivi karibuni yaliyotokea katika mji huo, yaligharimu maisha ya watu saba na makumi kujeruhiwa.

Askari wengi walitumwa Jumatano huko Dabou kujaribu kurejesha utulivu Mji huu unakumbwa na mapigano na visa vya uporaji. Milio ya risasi imeendelea kusikika. Tangu mwanzoni mwa wiki hii mjii huu umeendelea kushuhudia ongezeko la vurugu.

Siku ya Jumatatu, vizuizi viliwekwa kweye barabara mbalimbali na matukio kadhaa ya makabiliano yaliripotiwa. Wakati huo watu wasiopungua watatu walipoteza maisha. Miongoni mwao, kijana mwenye umri wa miaka ishirini aliuawa kwa panga katika kijiji cha Kpass nje kidogo ya mji wa Dabou.

Siku ya Jumatano, vijana kutoka vijiji jirani walivamia vitongoji vya Malinke kwa kile kilichoonekana kama shughuli za kulipiza kisasi. Jioni, viongozi walihesabu angalau vifo vipya vinne, kwa jumla ya watu saba waliopoteza maisha na makumi ya waliojeruhiwa kwa muda wa saa 48 zilizopita.

Hali ya usalama bado ni tete katika mji wa Dabou, Magharibi mwa Cote d'Ivoire.