GUINEA-SIASA-USALAMA

Hali ya wasiwasi yatanda Guinea kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya awali

Nchini Guinea, Tume ya Uchaguzi imekuwa ikitangaza sehemu ya matokea ya uchaguzi uliofanyika Jumapili, kutoka majimbo tofauti nchini Guinea.

Mji wa Conakry ulikumbwa na hali ya sintofahamu Jumatano Oktoba 21.
Mji wa Conakry ulikumbwa na hali ya sintofahamu Jumatano Oktoba 21. Reuters
Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya awali katika ngazi ya taifa bado hayajajulikana kwa uchaguzi huu ambao ulifuatiwa na vurugu huko Conakry na miji mingine ya nchi katika siku za hivi karibuni.

Siku ya Alhamisi hii, Oktoba 22, serikali ya Guinea na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini humo walikutana saa chache kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi.

Mkutano huo wa faragha ulifanyika kwenye makao makuu ya Wizara ya Mambo ya nje. Waziri wa Mambo ya Nje wa Guinea alikumbusha kwamba waangalizi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS, walipongeza jinsi uchaguzi huo ulifanyika. Kulingana na waziri huyo, tangazo la Cellou Dalein Diallo, kutangaza kuwa ameibuka mshindi wa uchaguzi, ndio chanzo cha vurugu zote za siku za hivi karibuni.

Chama cha upinzani cha UFDG kilitoa matokeo yake Jumatano, kikidai kukusanya zaidi ya asilimia 84 ya taarifa kutoka vituo vya kupigia kura, kwa kutumia mfumo wa kutuma ujumbe mfupi, skana za kupigia kura na kituo cha kupiga simu. Waziri wa Mambo ya nje alisema programu hiyo imetupwa na wakati na kutangaza uwezekano wa kumfungulia mashitaka.