MALI-USALAMA

Jeshi la Mali latuhumiwa kutekeleza mauaji katika mkoa wa Mopti

Wanajeshi wa Mali wanatuhumiwa kuwapiga risasi hadi kufa wanakijiji katika eneo la Bankass.
Wanajeshi wa Mali wanatuhumiwa kuwapiga risasi hadi kufa wanakijiji katika eneo la Bankass. MICHELE CATTANI / AFP

Wiki iliyopita, mashambuliei matatu ya kundi la GSIM linalodai kutetea Uislamu na Waislamu, lenye mafungamano na kundi la Al-Qaeda yalilenga kambi ya jeshi ya Sokoura na kisha raia, na kuua jumla ya watu 24 , kulingana na ripoti ya jeshi la Mali.

Matangazo ya kibiashara

Tangu wakati huo jeshi la Mali lilizindua operesheni kabambe dhidi ya magaidi katika eneo hilo. Operesheni ambayo imegubikwa na dhuluma, kulingana na vyanzo kadhaa kutoka mkoa wa Mopti.

"Operesheni kubwa", kulingana na jeshi la Mali, inaendelea "katika milima ya Dogon na eneo la Seno". Operesheni ya kupambana na ugaidi baada ya mashambulizi mawili wiki iliyopita, moja kwenye kambi ya jeshi ya Sokoura, ambapo wanajeshi 11 waliuawa, na lingine dhidi ya basi la raia, watu 13 walipoteza maisha, kulingana na ripoti rasmi.

Operesheni hii inakusudia "kulinda raia na kupambana na ugaidi" limeeleza jeshi la Mali, bila kutoa maelezo zaidi juu ya vitendo vinavyoendelea.

Lakini shirika la haki za binadamu kwa jamii za wafugaji huko Sahel, KISAL, linashtumu jeshi la Mali kwa kutekeleza mauaji dhidi ya watu kutoka jamii ya Fulani. Kijiji cha Libbé, katika eneo la Bankass, kilishambuliwa siku ya Alhamisi mchana: karibu miili kumi na tano ilipatikana, karibu nyumba zote zilichomwa moto, na wakazi ikiwa ni pamoja na mkuu wa kijiji, walilazimika kuyatoroka makaazi yao.

Kwa upande wake jeshi la Mali limetupilia mbali madai haya, yaliyoelezewa na msemaji wake kama "propaganda."