GUNIEA-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Guinea: Alpha Condé atangazwa mshindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi

Tume ya Uchaguzi nchini Guinea imemtangaza rais anayemaliza muda wake Alpha Condé kuwa ameibuka mshindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi kwa 59.49% ya kura.

Mwanamke huyu akiweka kura yake katika sanduku la kupigia kura wakati wa uchaguzi wa urais nchini Guinea huko Conakry Septemba 18, 2020.
Mwanamke huyu akiweka kura yake katika sanduku la kupigia kura wakati wa uchaguzi wa urais nchini Guinea huko Conakry Septemba 18, 2020. AP Photo/Sadak Souici
Matangazo ya kibiashara

Mpinzani wake Cellou Dalein Diallo, ambaye alijitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo hayo, amepata 33.5% ya kura, kulingana na Tume ya Uchaguzi (CENI).

Matokeo hayo ni ya awali, kwa kusubiri Mahakama ya Katiba kuthibitisha au la ushindi huo.

Matokeo ya awali ya uchaguzi yametangazwa na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (Céni). Baada ya zoezi la uhesabuji wa kura katika siku za hivi karibuni, rais anayemaliza muda wake Alpha Condé na chama chake cha RPG Arc-en-Ciel, wameshinda uchaguzi kwa 59.41% ya kura. Amemshinda mpinzani wake mkuu Cellou Dalein Diallo kutoka chama UFDG kwa 33% ,ameripoti mwandishi wetu aliyetumwa huko Conakry, Charlotte Idrac.

"Huu ni mwisho wa wakati wa kihistoria," amesema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kabinet Cissé, ambaye amebaini kwamba wapiga kura waliojitokeza katika duru ya kwanza ya uchaguzi walikuwa 78.9%.

Wakati huo huo kiongozi wa upinzani Cellou Dalein Diallo amefutilia mbali matokeo hayo na kusema kuwa ni ushindi wa Alpha Conde sio halali, akishtumu Tume ya Uchaguzi, CENI, kumpa kura zisizo halali rais Conde. Amessema kuwa atawasilisha malalamiko yake mbele ya Mahakama ya Katiba.

Wakati hayo yakiarifiwa kambi ya Alpha Conde imeendelea kusherehekea ushindi wao usiku kucha.