GUINEA-SIASA-USALAMA

Guinea: Ujumbe wa kidiplomasia wa pande tatu wakutana na Cellou Dallein Diallo

Kiongozi wa upinzani nchini Guinea Cellou Dalein Diallo anapiga kura huko Conakry, Oktoba 18, 2020.
Kiongozi wa upinzani nchini Guinea Cellou Dalein Diallo anapiga kura huko Conakry, Oktoba 18, 2020. AP Photo/Sadak Souici

Ujumbe wa pamoja wa pande tatu, Umoja wa Mataifa-Umoja wa Afrika-Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, umekuwa Conakry tangu Jumapili kujaribu kupata suluhisho la mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kukutana na maafisa kutoka Tume ya Uchaguzi, CENI, serikali, na balozi kutoka nchi za kigeni nchini humo Jumatatu, Oktoba 26, ujumbe huo ulikutana kwa mazungumzo na kiongozi wa upinzani Cellou Dalein Diallo nyumbani kwake.

Wakati huo huo, hali ya utulivu imerejea katika mji mkuu wa Guinea, Conakry. Idadi ya watu waliouawa katika machafuko hayo ya baada ya uchaguzi sasa imefikia 21 kwa mujibu wa serikali, karibu 30 kulingana na chama cha upinzani cha UFDG.

Awali Cellou Dalein Diallo alitaka kukutana na ujumbe huo katika makao makuu ya chama chake, lakini mazungumzo hayo yalifanyika nyumbani kwake, katika wilaya ya Dixinn, ambapo wakati huo makazi yake yalizingirwa na vikosi vya ulinzi na usalama vinavyodhibiti barabara zinazoingia nyumbani kwake.

Ujumbe huo wa pande tatu uliwasihi wanasiasa nchini Guinea kuzingatia amani na usalama wa nchi yao, na kuweka kando tofauti zao kwa maslahi ya taifa.

Hata hivyo Cellou Dalein Diallo amesema "hakutarajia mengi kutoka kwa wajumbe hao", ambao, amesema, "wameendelea kumuunga kono Alpha Condé".

Mara tu baada ya mkutano huo, chama cha UFDG kilidai kwamba manaibu viongozi wake wawili, Fodé Oussou Fofana na Kalemodou Yansané, walikamatwa na polisi. Mkutano wa ujumbe huo na waandishi wa habari, uliokuwa umepangwa kufanyika Jumatatu jioni, umeahirishwa.