NIGER-USALAMA

Raia mmoja wa Marekani atekwa nyara Kusini mwa Niger

Massalata, kilomita 400 mashariki mwa Niamey karibu na mpaka na Nigeria.
Massalata, kilomita 400 mashariki mwa Niamey karibu na mpaka na Nigeria. Studio graphique FMM

Raia mmoja wa Marekani ametekwa nyara mapema leo Jumanne Kusini mwa Niger na kundi la watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki, vyanzo vilivyo karibu na idara za usalama na mamlaka nchini humo vimebaini.

Matangazo ya kibiashara

Utekaji nyara huo ulifanyika karibu saa saba usikuwa kuamkia leo Jumanne katika kijiji cha Massalata, karibu na mji wa Birnin Konni, kwenye mpaka na Nigeria, vyanzo hivyo vimeongeza.

Mateka huyo alikuwa anaishi na kaka yake na dada yake katika eneo hili kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo walinunua sehemu ya ardhi na kujenga nyumba, amesema mkuu wa mji wa Birnin Konni, Abba Lele.

Baba wa mtu huyo aliyetekwa nyara pia anaishi katika kijiji cha Massalata tangu mwaka 2003. Wanafuga ngamia ambao mara nyingi hutembea msituni. Watu wengine wa familia yake walifungwa kamba na washambuliaji na polisi ilipewa taarifa saa nne baadaye.

Viongozi wanaamni kwamba raia huyo wa Marekani amepelekwa katika nchi jirani ya Nigeria, ameongeza Abba Lele.

Mji wa Birnin Konni unapatikana karibu kilomita 200 mashariki mwa mji mkuu na kilomita mia chache magharibi mwa kona ya kusini-mashariki mwa Niger, eneo ambalo mara kadhaa limekuwa likilengwa na wapiganaji wa Boko Haram.

Angalau mateka sita wa kigeni wanashikiliwa na waasi wa Kiislam nchini Mali, Burkina Faso na Niger.Wawili kati yao walitekwa nyara nchini Niger. Wawili hao ni Mmarekani Jeffery Woodke, ambaye alitoweka mnamo mwezi Oktoba 2016, na mfanyakazi wa shirika la kutoa msaada kutoka Ujerumani Jörg Lange, ambaye alitekwa nyara mnamo mwezi Aprili 2018 karibu na kijiji kilio karibu na mpaka wa Mali.