COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA

Côte d'Ivoire yafanya uchaguzi, hali ya wasiwasi yatanda Bouaké na Abidjan

Siku moja kabla ya uchaguzi Oktoba 31, mvutano kati ya utawala na upinzani umeendelea kuwatia wasiwasi raia, hasa huko Bouaké na Abidjan (picha ya kumbukumbu).
Siku moja kabla ya uchaguzi Oktoba 31, mvutano kati ya utawala na upinzani umeendelea kuwatia wasiwasi raia, hasa huko Bouaké na Abidjan (picha ya kumbukumbu). © AFP/ISSOUF SANOGO

Karibu wapiga kura milioni 7.5 wanapiga kura leo Jumamosi Oktoba 31, kumchagua rais wao mpya. Lakini kunaripotiwa mivitano kati ya utawala na upinzani, hali ambayo inawatia wasiwasi raia wa nchi hiyo, hasa katika mji mkuu wa uchumi Abidjan na mikoani, kama vile huko Bouaké.

Matangazo ya kibiashara

Wengi wamenunua chakula kwa wingi kwa kuhofia kuwa huenda machafuko kama yale ya mwaka 2010 yakatokea.

Côte d'Ivoire imeendelea kukumbwa na maandamano ya upinzani dhidi ya muhula wa tatu wa rais Alassane Ouattara.

rais Ouattara aliamua kutetea kiti chake, baada ya mrithi wake Amadou Gon Coulibaly kufariki dunia Julai 8.

Kwa mwezi mmoja mfululizo, upinzani umeendelea kutoa madai yanayoeleweka kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wowote. Madai hayo ni pamoja na kuondolewa Alassane Ouattara kwenye orodha ya wagombea. Hatua ya Alassane Ouattara kuwania katika uchaguzi huo kwa muhula wa tatu ni kinyume na Katiba ya nchi, kulingana na upinzani.

Hivi karibuni wagombea wawili wa upinzani nchini Cote d'Ivoire wamejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais, wakati wa uchaguzi wa urais mwishoni mwa mwezi huu.

Wawili hao Henri Konan Bédié na Pascal Affi N'Guessan, walitoa tangazo hilo baada ya kuanza kwa kampeni za kutafuta uongozi wa nchi hiyo katika uchaguzi ambao rais Ouattara anawania kwa muhula wa tatu.

Tayari viongozi wa kidini wameendelea kutoa wito wa kudumisha umoja, huku wasanii wakinadi amani na kuwataka raia kuwa na uvumilivu.