TANZANIA- UCHAGUZI 2020

Licha ya ushindi wa kishindo, Magufuli akosolewa kwa kuminya Demokrasia

PICHA YA MAKTABA: Rais wa Tanzania, John Magufulim ambaye amechaguliwa kwa muhula wa pili, Nairobi, Kenya October 31, 2016.
PICHA YA MAKTABA: Rais wa Tanzania, John Magufulim ambaye amechaguliwa kwa muhula wa pili, Nairobi, Kenya October 31, 2016. REUTERS/Thomas Mukoya/File Photo

Magufuli ambaye juma hili alifikisha umri wa miaka 61, hapo jana alifanikiwa kushinda muhula wa pili madarakani kwa kupata asilimia 84 ya kura zote, katika uchaguzi ambao upinzani umesema hautambui ushindi wake.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mara ya kwanza alichaguliwa mwaka 2015 baada ya kujipambanua kama mpinga vitendo vya rushwa ambapo alipata uungwaji mkono mkubwa toka kwa wananchi na kuchaguliwa.

Punde baada ya kuingia madarakani akapata umaarufu baada ya kufuta sherehe za uhuru na kusitisha safari za nje ya nchi kwa viongozi wa uma pamoja na kuwabana na hata kuwafukuza kazi mawaziri na viongozi wengine alioona wanazembea kazini.

Hata hivyo baadhi ya hatua alizokuwa akiziuchukua, hazikuyapendeza baadhi ya mataifa ya kigeni na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, yaliyoona ni kama anaminya demokrasia katika moja ya taifa ambalo lilikuwa likisifika duniani kwa kuwa na utulivu na kuheshimika kimataifa.

Matukio kadhaa ambayo yalionesha kuigusa Jumuiya ya kimataifa ni pamoja na kuzuia mikutano ya kisiasa baada ya kuchaguliwa, kupitisha sheria ya bunge kuzuiwa kuoneshwa mubashara na sheria kadha zenye utata kuhusu huduma za vyombo vya habari.

Kauli yake ya kutaka wasichana wa shule watakaopata ujauzito kufukuzwa ni miongoni mwa kauli ambazo ziliishtua dunia.

Miezi kadhaa nyuma, licha ya nchi wanachama za Afrika Mashariki kufunga mipaka yake kutokana na janga la Corona, rais Magufuli alitangaza nchi yake kuwa huru kutokana na ugonjwa huo huku hadi sasa kukiwa hakuna takwimu sahihi kuhusu ilivyokuwa mwenendo wa ugonjwa huo.

Hata hivyo kwa wafuasi wa chama tawala CCM, rais Magufuli ni mkombozi wa wanyonge na pengine ndio sababu ya kuchaguliwa kwake kwa kishindo.