COTE D'IVOIRE-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Cote d'Ivoire: Rais Ouattara aibuka mshindi wa uchaguzi wa urais kwa muhula wa tatu

Alassane Ouattara wakati wa mkutano wa chama chake cha RHDP huko Abidjan, Julai 20, 2020.
Alassane Ouattara wakati wa mkutano wa chama chake cha RHDP huko Abidjan, Julai 20, 2020. SIA KAMBOU / AFP

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi usiku wa Jumatatu kuamkia leo Jumanne, Alassane Ouattara ameibuka mshindi kwa 94.27% ya kura kwa duru ya kwanza ya uchaguzi.

Matangazo ya kibiashara

Tume Huru ya Uchaguzi (CEI) imetangaza usiku wa Jumatatu kuamkia leo Jumanne matokeo kamili ya awali ya uchaguzi wa urais uliyofanyika Jumamosi, Oktoba 31. Alassane Ouattara ndiye mshindi kwa kura 94.27% ya kura. Pascal Affi N’guessan amepata 0.99% ya kura.

Henri Konan Bédié amepata 1.66% na Kouadio Konan Bertin amepata 1.99% ya kura kulingana na takwimu hizi rasmi. Kiwango cha ushiriki kulingana na IEC ni 53.90%. Matokeo haya yanatarajiwa kuthibitishwa na Mahakama ya Katiba.

Upinzani nchini Cote d'Ivoire, ambao ulisusia uchaguzi wa urais, ulitangaza siku ya Jumatatu kwamba utaunda serikali ya mpito siku mbili baada ya uchaguzi uliyogubikwa na machafuko.

Wakati huo huo milio ya risasi ilisikika jana usiku karibu na nyumba za viongozi kadhaa wa upinzani, kama vile Henri Konan-Bédié, Pascal Affi N'Guessan, Albert Toikeusse-Mabri au hata Assoa Adou. Mpaka sasa hakuna taarifa za majeruhi ambazo zimeripotiwa.