DRC-USALAMA

DRC: Mfanyabiashara maarufu Simba Ngezayo auawa kwa kupigwa risasi Goma

Picha ya Mji wa Goma nchini DRC
Picha ya Mji wa Goma nchini DRC RFI/Leonora Baumann

Wafanyabiashara wakubwa wameendelea kulengwa na mashambulizi ya watu wenye silaha katika mji mkuu wa mkoa aw Kivu Kaskazini, Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Hali ya usalama katika mji huo imedorora, kwani uhalifu huu mara nyingi hufanywa wakati wa mchana.

Jumanne wiki hii mfanyabiashara maarufu Simba Ngezayo aliuawa kwa kupigwa risasi na kundi la watu wawili wenye silaha. Wauaji wake bado hawajapatikana na uchunguzi umeanzishwa.

Tukio hilo lilitokea saa 7.20 asubuhi. Mfanyabiashara huyo alikuwa akiongozana na mtoto wake kwenda shuleni alipopigwa risasi na watu wawili wasiojulikana waliokuwa awlijihami kwa silaha.

Kulingana na polisi na mashuhuda, wauaji hao walimpiga risasi kadhaa kabla ya kutoweka kwa pikipiki.

Simba Ngezayo ni mfanyabiashara mashuhuri huko Goma. Familia yake ni miongoni mwa matajiri wakubwa katika jiji la Goma. Baba yake, Victor, ni mmiliki wa moja ya hoteli kubwa zaidi katika eneo hilo. Jina la Ngezayo limekuwa liligonga vichwa vya habari kwenye magazeti kwa miezi kadhaa kufuatia mzozo wa ardhi unaohusiana na hoteli ambayo Ngezayo anasimamia. Miaka mitatu iliyopita, mjomba wa Simba Ngezayo alipigwa risasi na kuuawa mchana kweupe katika mazingira kama hayo.

Mashambulizi ya watu wenye silaha dhidi ya wafanyabiashara wakubwa na wafanyabiashara wengine wa kawaida yanaendelea kuripotiwa huko Goma.

Wanaharakati wa mashirika ya kiraia wanabainisha kuwa mauaji haya mara nyingi yanahusiana na mizozo ya ardhi na usimamizi mbaya wa utaratibu wa kuwapokonya silaha na kuwarejesha katika maisha ya kiraia wapiganaji wa zamani, ambao baadhi yao huajiriwa na makundi ya uhalifu huko Goma.