COTE D'IVOIRE-SIASA-USALAMA-HAKI

Côte d'Ivoire: Wapinzani Mabri na N'Guessan wasakwa na mahakama

Viongozi wa upinzani nchini Côte d'Ivoire, Pascal Affi N’Guessan na Albert Toikeusse Mabri, wanatafutwa na mahakama nchini humo kwa ushiriki wao katika uamuzi wa kuanzishwa kwa "Baraza la Mpito la Kitaifa" Novemba 2.

Pascal Affi N'Guessan, kiongozi wa chama cha Ivorian Popular Front (FPI) na mgombea urais mwaka 2020, wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Abidjan, Novemba 1, 2020.
Pascal Affi N'Guessan, kiongozi wa chama cha Ivorian Popular Front (FPI) na mgombea urais mwaka 2020, wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Abidjan, Novemba 1, 2020. Luc Gnago/Reuters
Matangazo ya kibiashara

Pascal Affi N’Guessan na Albert Toikeusse Mabri wanashtumiwa makosa yanayohusiana na mashambulizi na kula njama dhidi ya mamlaka, mwendesha mashtaka aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa (Novemba 6).

Mbele ya waandishi wa habari, mwendesha mashtaka wa Abidjan Richard Adou alitoa maelezo kadhaa juu ya kukamatwa kwa wapinzani kadhaa katika siku za hivi karibuni. Mnamo Novemba 3, siku moja baada ya tangazo la kuanzishwa kwa "Baraza la Mpito la Kitaifa", karibu watu 20 walikamatwa nyumbani kwa Henri Konan Bédié.

Tisa waliachiliwa huru. Lakini kumi na wawili bado wako mikononi mwa mahakama, pamoja na naibu kiongozi wa chama cha PDCI, Maurice Kakou Guikahué. Kiongozi wa chama cha FPI, Pascal Affi N'Guessan, ambaye alitangaza kwa niaba ya upinzani kuanzishwa kwa baraza hilo la Mpito la Kitaifa, na kiongozi wa chama cha UDPCI, Albert Toikeusse Mabri, "wako mafichoni na wanatafutwa kikamilifu", kulingana na mwendesha mashtaka.

Richard Adou amesema kwa kuunda "Baraza la Mpito" na kutangaza serikali yao, viongozi wa upinzani walifanya kitendo cha uchochezi "ninachohusiana na makosa ya mashambulizi na njama dhidi ya mamlaka na uhuru wa taifa ”. Lakini upande wa mashtaka haukusubiri tangazo la Baraza la Mpito la Kitaifa kwa kuanzisha uchunguzi.