LIBYA-UN-USALAMA-SIASA

Libya: Tofauti zajitokeza kwa mara ya kwanza wakati wa ufunguzi wa mazungumzo Tunis

Wawakilishi wa pande pinzani nchini Libya, wameanza mazungumzo ya amani nchini Tunisia tangu Jumatatu wiki hii, chini ya Umoja wa Mataifa, lengo likiwa ni kurejesha utrulivu katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Washiriki katika Mazungumzo ya kisiasa nchini Libya. Novemba 9, 2020 huko Tunis
Washiriki katika Mazungumzo ya kisiasa nchini Libya. Novemba 9, 2020 huko Tunis REUTERS/Zoubeir Souissi
Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo haya katika nchi hiyo jirani ya Tunisia yanakuja baada ya nchi hiyo kushuhudia utulivu kuanzia mwezi Oktoba baada ya viongozi wa serikali jijini Tripoli na wale wa upinzani kukubali kuweka silaha chini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress amewaambia wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo kuwa, wana nafasi ya kipekee ya kumaliza mzozo ambao umekuwa ukiendelea katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Baada ya maelewano ya mwezi Oktoba ya kusitisha mapigano, nchi hiyo ilianza tena kuchimba mafuta na wajumbe 75 kutoka nchini Libya wanaokutana katika mji wa Gammarth, wana matumaini ya kupata suluhu ya kudumu.

Tangu mwaka 2011, Libya imeshuhudia ukosefu wa usalama baada ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Moamer Kadhafi, ambapo serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, imekuwa ikikabiliana na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar kudhibiti nchi hiyo.