TANZANIA

Tundu Lissu aondoka nchini Tanzania, baada ya kukimbilia ubalozi wa Ulaya

Aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, hivi leo ameondoka nchini humo kuelekea Ujerumani, baada ya kuwa amepewa hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu juma moja lililopita.

Aliyekuwa mgombea wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, qnqyepungq mkono, hii ni baada ya kuidhinishwa na chama chake cha Chadema
Aliyekuwa mgombea wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, qnqyepungq mkono, hii ni baada ya kuidhinishwa na chama chake cha Chadema CHADEMA Tanzania/twitter.com
Matangazo ya kibiashara

Siku chache baada ya kutoa taarifa kuhusu kutotambua matokeo ya uchaguzi mkuu wa Octoba 28 ambapo rais John Magufuli, alichaguliwa kuhudumu kza muhula wa pili na wa mwisho, Lissu alikimbilia ubalozi wa umoja wa Ulaya kuomba hifadhi akidai kuhofia maisha yake.

Juma lililopita, alikamatwa na vyombo vya usalama saa chache tu baada ya kutoka katika ofisi za umoja wa Ulaya jijini Dar es Salaam, ambapo alikutana na balozi wa Ujerumani kabla ya kumpa hifadhi nyumbani kwake.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, wanasiasa kadhaa wa upinzani wameripoti kuhofia maisha yao kwa kile walichodai wamekuwa wakipokea vitisho.

Tundu Lissu alirejea nchini mwake mwaka huu baada ya miaka karibu mitatu kuwa nje ya nchi kwa matibabu, baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa bungeni nchini Dodoma mwaka 2017.

Tangu wakati huo Lissu, amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Magufuli, akiituhumu kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo kuminya uhuru wa vyombo vya habari na kufanya siasa.

Kuondoka kwake nchini Tanzania, kunakuja wakati huu pia wanasiasa kadhaa wakiripotiwa kupanga kuondoka nchini humo kwa kile wanachosema wanahofia usalama wao.

Tukio la hivi karibuni ni kukimbia kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema, ambaye juma hili aliruhusiwa kuingia nchini Kenya kuomba hifadhi ya kisiasa.

Juma lililopita kulikuwa na taarifa pia wa mbunge wa zamani wa chama tawala, Lazaro Nyalandu, kuzuiliwa katika mpaka wa Namanga, wakati akijaribu kuingia nchini Kenya.

Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu, ikiwemo Amnesty International na Human Rights Watch, walitoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuheshimu haki za binadamu ikizemo kuacha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wakosoaji wa Serikali ya rais Magufuli.

Tangu rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, alipiga marufuku mikutano ya kisiasa, hatua iliyokosolewa vikali na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wakisema ni kuminya uhuru wa kufanya siasa.

Mbali na mikutano ya kisiasa, Serikali yake imekuwa ikikosolewa na mashirika ya kimataifa kuhusu kuminya uhuru wa vyombo vya habari, ambapo kwa miaka miwili iliyopita bunge lilitunga sheria kadhaa wa kudhibiti vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.