AFRIKA KUSINI-ANC-UFISADI-SIASA-UCHUMI

Afrika Kusini: Katibu mkuu wa chama cha ANC alengwa na waranti wa kukamatwa kwa ufisadi

Katibu Mkuu wa ANC Ace Magashule, mtu maarufu katika chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, anakabiliwa na waranti wa kukamatwa. Anashtumiwa makosa yanayohusiana na rushwa katika kesi ya kandarasi ya umma ya tangu alipokuwa gavana wa jimbo la Free State.

Katibu Mkuu wa chama cha ANC Ace Magashule huko Johannesburg, Februari 2018.
Katibu Mkuu wa chama cha ANC Ace Magashule huko Johannesburg, Februari 2018. GIANLUIGI GUERCIA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Hii ni moja ya kashfa nyingi zinazozidi kusababisha chama cha ANC kugawanyika.

Uvumi wa uwezekano wa waranti wa kukamatwa dhidi ya Ace Magashule ulikuwa ukisambaa kwa wiki moja sasa. Siku ya Jumanne, polisi walithibitisha kuwepo na waranti huo ambao umesainiwa. Polisi pia imetangaza kwamba katibu mkuu wa chama cha ANC anatarajiwa kufika mahakamani Ijumaa wiki hii.

Mashtaka dhidi yake ni ya tangu mwaka 2014. Yanahusiana na kandarasi ya kiasi cha takriban dola milioni 15 ya kukarabati baadhi ya barabara na majengo kadhaa ya serikali katika kitongoji duni cha mkoa wa Free State.

Ace Magashule alikuwa akifanya kampeni katika mji mmoja huko Soweto Jumanne wiki hii kujiandaa kwa uchaguzi ujao wakati habari hii ilivuja, kwanza kupitia vyombo vya habari. Mbele ya waandishi wa habari, katibu mkuu wa chama cha ANC alijibu kwamba bado hajaarifiwa juu ya waranti wa kukamatwa, na kusema kwamba hana hatia, huku akibaini yuko tayari kukanusha tuhuma dhidi yake mbele ya mahakama". "Adui" amejipenyeza kwa chama tawala, amesema pia.

Chama cha ANC kinachozidi kugawanyika. Ndani ya chama cha ANC, Ace Magashule ni kutoka kambi ambayo imeendelea kuwa karibu na rais wa zamani Jacob Zuma na ambao inapinga ile ya rais wa sasa Cyril Ramaphosa. Tangu kuingia kwake madarakani, rais ramaphosa amekuwa akijaribu kurejesha sura ya chama hiki kilichochafuliwa na mfululizo wa kashfa zilizorudiwa ambazo zilikuwa zimekithiri kwa miaka 9 katika utawala wa mtangulizi wake.