ETHIOPIA-USALAMA

Ethiopia: Mapigano yaendelea kurindima katika jimbo la Tigray

Askari wa vikosi vya Amhara anapiga doria katika mitaa ya kijiji cha Soroka, karibu na mpaka wa jimbo la Tigray, Novemba 9, 2020.
Askari wa vikosi vya Amhara anapiga doria katika mitaa ya kijiji cha Soroka, karibu na mpaka wa jimbo la Tigray, Novemba 9, 2020. REUTERS/Tiksa Negeri

Jimbo la Tigray, Kaskazini mwa Ethiopia, ambalo linaendelea kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa wiki moja sasa, kukumbwa na hali ya sintofahamu baada ya barabara kuzfungwa na mawasiliano kukatwa. Ni vigumu kujua kinachoendelea katika jimbo hilo la kihistoria ambalo halijukani sana.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia amedai kwamba majeshi ya Eritrea yamevuka na kuyashambulia majeshi ya jimbo hilo baada ya vikosi vya serikali kuu ya waziri mkuu Abiy Ahmed kuanzisha mashambulizi ndani ya Tigray wiki iliyopita.

Kulingana na wanadiplomasia, maafisa wa usalama na wafanyakazi wa mashirika ya misaada, mapigano yamesambaa kwenye mpaka kati ya jimbo la Tigray na jimbo la Amhara, ambalo linaunga mkono serikali kuu ya Ethiopia, karibu na mpaka na Sudan na Eritrea.

Siku ya Ijumaa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitangaza kwamba wanajeshi wa serikali kuu ya Addis Ababa waliuweka kwenye himaya yao mji wa Dansha ktoka mikononi mwa vikosi vya Tigrayvya People's Liberation Front (TPLF).

Katika tamko lake, kwa njia ya televisheni kiongozi wa Tigray Debretsion Gebremichael ameinyooshea kidole cha lawama Eritrea kwa kuwatuma askari wake katika imbo lake.

"Tangu jana majeshi ya Eritrea yamevuka mpaka na kulivamia jimbo la Tigray na yanatumia silaha nzito, " amesema Debretsion Gebremichael.

Mpaka sasa serikali ya Eritrea haijasema chochote, ingawa mwishoni mwa wiki iliyopita, waziri wake wa mambo ya nje alisema hakuna mwanajeshi wa nchi hiyo aliyevuka mpaka na kuingia nchini Ethiopia.