ANGOLA-MAANDAMANO-USALAMA-UMASIKINI

Angola: Makabiliano makali yatokea kati ya polisi na waandamanaji dhidi ya umasikini Luanda

Polisi imelazimika kufyatua risasi za moto na kutumia mabomu ya machozi dhidi ya vijana walioandamana kupinga umasikini katika mji mkuu wa Angola, Luanda.

Vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji huko Luanda, Angola, Novemba 11, 2020.
Vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji huko Luanda, Angola, Novemba 11, 2020. Osvaldo Silva / AFP
Matangazo ya kibiashara

Ni wiki kadhaa tangu maandamano dhidi ya serikali kuendelea kuripotiwa katika mji mkuu Luanda. Maandamano ya kupinga kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, maisha kuwa ghali, na ufisadi wa serikali. Matatizo yanayochochewa na janga la Corona.

Angola inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi, kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, lakini pia, kulingana na wachumi, na usimamizi mbaya wa mapato ya mafuta chini ya enzi ya rais wa zamani José Éduardo dos Santos.

Kiongozi mpya wa nchi hiyo, Joao Lourenço, aliyeingia madarakani miaka mitatu iliyopita, alianzisha mpango wa mageuzi ya kiuchumi, lakini janga la Corona limesababisha hali kuwa mbaya zaidi, rais Joao Lourenço alikiri Jumatano jioni.

"Kwa bahati mbaya, kuna watu ambao wanajaribu kunufaika kisiasa kupitia hali hii ya kiafya, wakati mgogoro hu wa kiafya unayakumba mataifa mengi duniani. Mgogoro huu hakukuletwa kwa usimamizi mzuri au mbaya wa serikali. Hatua tulizochukuwa zinalenga kuokoa maisha ya watu. Na Waangola wanapaswa kuzingatia na kuheshimu hatua hizo " , amesema rais Lourenço.

Upinzani, ambao unaunga mkono maandamano hayo, pia unataka kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa. uchaguzi huo ulikuwa lumepangwa kufanyika mwaka huu, lakini umeahirishwa kwa sababu ya janga la Covid-19.