GHANA-SIASA-USALAMA

Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings aaga dunia akiwa na umri wa miaka 73

Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings.
Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings. REUTERS

Rais wa zamani wa Ghana, Jerry Rawlings, aliyeingia madarakani kufuatia mapinduzi mawili ya kijeshi kabla ya kuanzisha utawala wa kidemokrasia nchini mwake, amefariki dunia leo Alhamisi asubuhi akiwa na umri wa miaka 73, kulingana na chanzo kutoka ikulu.

Matangazo ya kibiashara

Jerry Rawlings, wakati huo akiwa Luteni katika kikosi cha jeshi la wanaanga, alimpindua Jenerali Frederick Akuffo mnamo mwaka 1979 na kuongoza nchi ya Ghana kwa kipindi kifupi na kisha kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia kabla ya kufanya mapinduzi mengine miaka miwili baadaye, akibaini kwamba serikali ilishindwa kukomesha ufisadi na hakukuwa na uongozi bora.

Kuanzia mwaka 1981 hadi 1993, Jerry Rawlings aliongoza serikali iliyoundwa na wanajeshi na raia. Mnamo 1992, alichaguliwa kuwa rais wa Jamhuri chini ya katiba mpya na alichukua madaraka mwaka uliofuata kwa mihula miwili kabla ya kukabidhi madaraka kwa John Kufour mnamo mwaka 2001.

Hakuna maelezo yaliyotolewa juu ya mazingira ya kifo cha Jerry Rawlings.