BURKINA FASO-MAUAJI-USALAMA

Burkina Faso: Wanajeshi kumi na wanne wauawa siku chache kabla ya uchaguzi

Idadi ya askari waliouawa kaskazini mwa Burkina Faso Jumatano wiki hii inaendelea kuongezeka. Wanajeshi kumi na wanne wa Burkina Faso waliuawa wakati nchi hiyo ikiwa katika kampeni za uchaguzi wa urais na wa wabunge wa Novemba 22.

Wanajeshi wa Burkina Faso wakati wa mafunzo ya kijeshi Aprili,13,  2018 (picha ya kumbukumbu).
Wanajeshi wa Burkina Faso wakati wa mafunzo ya kijeshi Aprili,13, 2018 (picha ya kumbukumbu). ISSOUF SANOGO / AFP
Matangazo ya kibiashara

Shambulio hilo lilitokea kati ya mji wa Beldiabe na Tin-Akoff. "Washambuliaji walikuwa wengi wakati waliposhambulia kituo hicho cha jeshi, huku wakijihami kwa silaha za kivita," kimesema chanzo cha usalama.

Kulingana na chanzo hicho, kikosi cha wanajeshi kilikuwa kimeondoka katika eneo la Gorom-Gorom na kurudi tena katika kituo chake huko Tin-Akoff, karibu na mpaka wa Mali.

Kutokana na shambulio hili baya, wagombea kadhaa wameamua kuditisha kampeni zao kwa siku kadhaa.

Wakati wa mkutano mkubwa mbele ya wakazi wa mji wa Ziniaré, rais Kaboré aliomba kusalia kimya kwa dakika moja kuwakumbuka askari walioangamia katika shambulio hilo, hata kabla ya kutangazwa idadi rasmi ya waliouawa katika shambulio hilo. Dakika chache baadaye, alitangaza kusitisha kampeni yake kwa masaa arobaini na nane.

Kiongozi wa upinzani Zéphirin Diabré Tahirou Barry na wafuasi wa Yacouba Isaac Zida tangu wakati huo walichukua hatua kama hizo. Hakuna kampeni ya uchaguzi kwa muda wa saa ishirini na nne hadi sabini na mbili. Hii ni "kama ishara ya maombolezo na heshima kwa wanajeshi 14 waliouawa," amesema Zéphirin Diabré, mmoja wa viongozi wa upinzani.

Waziri Mkuu Christophe Dabiré amesema kusikitishwa na shambulio hili. "Licha ya matatizo tunayokabiliana nayo hususan shambulio hili, lazima tukamilishz mchakato wa uchaguzi na tuendeleze nchi yetu kuelekea maendeleo," ameongeza.