ETHIOPIA-USALAMA

Ethiopia: Amnesty International yalaani "mauaji ya raia" katika jimbo la Tigray

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limelaani mauaji ya raia wa kawaida katika jimbo la Tigray ambapo mapigano kati ya vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia na vikosi vya jimbo la Tigray, TPLF, yanaendelea kwa wiki kadhaa sasa.

Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele, nchini Ethiopia, Januari 25, 2018.
Mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele, nchini Ethiopia, Januari 25, 2018. Wikimedia Commons Copyleft A. Savin
Matangazo ya kibiashara

Hii ni mara ya kwanza kwa vifo vya idadi kubwa ya raia kuripotiwa tangu kuzuka kwa mzozo huo nchini Ethiopia. Mawasiliano kupitia njia ya simu bado yamekatwa, huku barabara zikiendelea kufungwa katika eneo hilo. Mzozo huo tayari umesababisha vifo vya mamia ya watu.

Mauaji hayo yalitokea usiku wa Novemba 9, katika mji wa Mai-Kadra, Kusini magharibi mwa jimbo la Tigray, kulingana na shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International.

"Watu wengi, labda mamia, wamechomwa visu au kuuawa kwa shoka," Amnesty International imesema katika taarifa.

Ni vigumu kuingia katika jimbo jilo, lakini shirika la Amnesty International linabaini kwamba lilitoa ripoti hiyo kulinagana na ushahidi kutoka kwa mashuhuda, picha za setilaiti, lakini pia picha na video zilizochunguzwa na kuthibitishwa, ambazo kunaonekana idadi kubwa ya "miili iliyotawanyika katika mji huo" au "kusafirishwa katika vyumba vya kuhifadhi maiti".

Kulingana na Deprose Muchena, mkurugenzi Amnesty International katika ukanda huo, mauaji hayo yalitekelezwa na vikosi vya jimbo la Tigray, TPLF, baada ya kushindwa dhidi ya vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema jeshi la Ethiopia limewashinda wanajeshi wa jimbo la Tigray huku akiwatuhumu wanajeshi hao kwa uhaini wakati wa mapigano yaliyodumu kwa wiki moja sasa na kutishia kuiyumbisha nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Katika ujumbe aliouandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Abiy amesema eneo la magharibi mwa Tigray liko huru sasa, kwa sasa jeshi linatoa misaada ya kiutu na kuwapa watu chakula.