DRC-ULINZI-USALAMA-SIASA

Mzozo kati ya Tshisekedi na Kabila: Jeshi la DRC lavunja ukimya na kuwaonya wanasiasa

Katikati ya mzozo kati ya Félix Tshisekedi na mtangulizi wake, Joseph Kabila, juu ya udhibiti wa taasisi muhimu, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) limeamua kuvunja ukimya wake, na kutoa msimamo.

Jeshi la FARDC likipiga doria katika eneo la Eringeti.
Jeshi la FARDC likipiga doria katika eneo la Eringeti. ALAIN WANDIMOYI / AFP
Matangazo ya kibiashara

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Alhamisi wiki hii, katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa, jeshi limeonyesha msimamo wake na kusema linaunga mkono taasisi za nchi hiyo, huku likionya wanasiasa na wale wanaotaka jeshi kuchukuwa hatua.

Ujumbe ukiwataka wanajeshi kuasi, ulirushwa katika siku za hivi karibuni, katika mitandao ya kijamii: malimbikizo ya malipo na marupurupu, ukosefu wa vifaa vya vita na hata mafuta. Jenerali Léon Richard Kasonga, msemaji wa jeshi la DRC amesema maneneo hayo yanaonyesha kwamba kuna watu ambao hawataki nchi hiyo kuwa na amani na kuendelea katika sekta lbalimbali: "FARDC inataka kusema kuwa kwa utendaji wao mzuri wa kazi, wanapokea mishahara yao na marupurupu yao, vifaa, mbalimbali vya kivita bila matatizo.

Hata hivyo Jenerali Léon Richard Kasonga amekiri kuepo na baadhi ya matatizo ,huku akisema kuwa yote hayo ni kutokana na janga la COVID-19.

"Kampeni hii inakusudia kugawanya wanajeshi na kuwataka waiasi serikali, kamwe hatutokubaliana na kauli hizi, " amesema Jenerali Léon Richard Kasonga.

"Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vinatoa wito kwa wanajeshi wote kuendelea kuwa wamoja, wenye nidhamu kama siku zote, na tuendelee kumuunga mkono amiri jeshi mkuu, rais wa jamhuri, " ameongeza msemaji wa jeshi la FARDC.