LIBYA-MAZUNGUMZO-SIASA-USALAMA

Libya: UN yatangaza makubaliano kuhusu uchaguzi kufanyika Desemba 24, 2021

Stephanie Williams, Kaimu Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, azungumza huko Tunis baada ya mazungumzo ya siku mbili, Novemba 11, 2020.
Stephanie Williams, Kaimu Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, azungumza huko Tunis baada ya mazungumzo ya siku mbili, Novemba 11, 2020. Fethi Belaid / AFP

Wajumbe kutoka makundi hasimu nchini Libya wanaokutana nchini Tunisia chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa wamefikia makubaliano kuhusu "uchaguzi katika ngazi ya kitaifa" kufanyika mnamo Desemba 24, 2021, Kaimu mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, MANUL.

Matangazo ya kibiashara

"Wadau wanaoshiriki mazungumzo ya Kisiasa nchini Libya wamekubaliana juu ya kufanyika kwa uchaguzi katika ngazi ya kitaifa mnamo Desemba 24, 2021," Williams amesema katika mkutano wa waandishi na habari.

Mazungumzo haya katika nchi hiyo jirani ya Tunisia yanakuja baada ya nchi hiyo kushuhudia utulivu kuanzia mwezi Oktoba baada ya viongozi wa serikali jijini Tripoli na wale wa upinzani kukubali kuweka silaha chini.

Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress aliwaambia wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo kuwa, wana nafasi ya kipekee ya kumaliza mzozo ambao umekuwa ukiendelea katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Baada ya maelewano ya mwezi Oktoba ya kusitisha mapigano, nchi hiyo ilianza tena kuchimba mafuta na wajumbe 75 kutoka nchini Libya wanaokutana katika mji wa Gammarth, wana matumaini ya kupata suluhu ya kudumu.

Tangu mwaka 2011, Libya imeshuhudia ukosefu wa usalama baada ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Moamer Kadhafi, ambapo serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, imekuwa ikikabiliana na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar kudhibiti nchi hiyo.