Msumbiji-USALAMA

Msumbiji: Cabo Delgado yakabiliwa na ukosefu wa usalama

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, anataka "hatua za haraka" zichukuliwe ili kulinda raia Kaskazini mwa Msumbiji.

Mama huyu na mtoto wake wamesimama mbele ya kijiji kimoja, karibu na mji wa Macomia (Cabo Delgado) baada ya shambulio, Agosti 24, 2019.
Mama huyu na mtoto wake wamesimama mbele ya kijiji kimoja, karibu na mji wa Macomia (Cabo Delgado) baada ya shambulio, Agosti 24, 2019. MARCO LONGARI / AFP
Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Novemba 13, rais wa zamani wa Chile anasema hali inaendelea kuwa mbaya katika mkoa wa Cabo Delgado, kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya wanajihadi wa kundi la al Shabab ambao wanadai kuwa wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu.

Tangu katikati ya mwezi Oktoba, mashambulizi yameongezeka katika mkoa wa Cabo Delgado. Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu kadhaa wamepoteza maisha yao, lakini hakuna idadi sahihi ambayo imetolewa.

Hivi karibuni watu wasiopungua ishirini waliangamia katika mauaji mapya katika eneo hilo la Kaskazini mwa Msumbiji.

Ni katika jimbo hili lenye utajiri mkubwa wa mafuta na linalopakana na Tanzania ambapo waasi wamekuwa watekeleza ghasia kwa miaka mitatu, baada ya kutangaza kujiunga na kundi la Islamic State.

Kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Armed Conflict Location & Event Data group, waasi wa Kiisilamu tayari wamehusika na vifo vya watu wasiopungua 2,000 tangu kuwasili kwao nchini Msumbiji na wamesababisha watu 400,000 kuyatoroka makaazi yao nchini humo.