ETHIOPIA-UN-USALAMA

UN: Mauaji katika jimbo la Tigray yanaweza kuwa uhalifu wa kivita

Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, ameonya kuwa madai ya mauaji nchini Ethiopia, ikiwa yatathibitishwa, yatakuwa uhalifu wa kivita.

Raia wa Ethiopia wakiyakimbia mapigano huko Tigray, Novemba 9, 2020.
Raia wa Ethiopia wakiyakimbia mapigano huko Tigray, Novemba 9, 2020. REUTERS/Tiksa Negeri
Matangazo ya kibiashara

Onyo hilo linakuja baada ya shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International kuripoti kwamba makumi ya raia waliuawa katika mji wa jimbo la Tigray.

Michelle Bachelet anataka uchunguzi kamili ufanyike na amesema wale waliohusika na makosa hayo iwapo yatathibitishwa lazima wawajibishwe.

Mamlaka katika jimbo la Tigray imekanusha madai kwamba vikosi vya jimbo la Tigray vilitekeleza mauaji hayo.

Bi Bachelet amebaini kwamba kipaumbele cha kwanza ni kumaliza mapigano.

Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba mzozo huo unaweza kuongezeka na hata kuenea mbali na mipaka ya Ethiopia.

Maelfu ya watu tayari wameyatoroka makazi yao na ukimbilia nchini Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea.

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema wengi wao ni watoto wanaofwasili wakiwa wamechoka.