CAMEROON-USALAMA-SIASA

Cameroon: Kardinali Tumi amtaka Paul Biya "atangaze msamaha"

Kardinali Christian Tumi, aliyetekwa nyara kwa muda mfupi na watu wasiojulikana hivi karibuni na kuachiliwa amevunja ukimya wake na kumtaka rais wa Cameroon kutangaza msamaha kwa wafungwa wote wa kisiasa wanaozuiliwa katika jela mbalimbali nchini humo.

Kardinali Christian Tumi mbele ya Kanisa Kuu la Douala mnamo 2004.
Kardinali Christian Tumi mbele ya Kanisa Kuu la Douala mnamo 2004. AFP / I. Sanogo
Matangazo ya kibiashara

Baada ya wiki moja ya mapumziko na kufanyiwa vipimo mbalimbali vya matibabu, kiongozi huyo wa kidini wa Cameroon, mwenye umri wa miaka 90 ameiambia RFI mkasa uliomkuta Novemba 5 na 6 nchini Cameroon na kusema kuwa alitekwa nyara lakini hakufanyiwa kibaya chochote kile.

Kardinali Christian Tumi alikamatwa na kisha kutekwa nyara kwenye barabara kati ya mji wa Bamenda na Kumbo, wakati alikuwa akisafiri akiandamana na Fon (mfalme wa jadi) wa jamii ya Nso, na watu kadhaa waliosindikiza.

Aliachiliwa siku iliyofuata. Katika eneo hilo la Kaskazini Magharibi, wanamgambo wa wanaotaka kujitenga wameendelea kuendesha harakati zao.

Kardinali Tumi ni maarufu nchini Cameroon kwa juhudi zake za kupatanisha wanaharakati wanaotaka kujitenga kutoka maeneo yanayozungumza Kiingereza na serikali ya Cameroon.

Kardinali Tumi ameimbia RFI kwamba waliomteka nyara walitaka kujua maoni yake kuhusu mfumo wa serikali ya Cameroon.

Niliwaambia: "huu ni ushirika. Walisema hapana [...] Ninaona kwamba rais wa jamhuri ndiye anatakiwa sasa kufanya kinachohitajika ili kukomesha hali hii, na nina imani kuwa anaweza kufanya hivyo, nikimaanisha kwamba anaweza kutoa msamaha ili kuwepo na amani na watoto waenda shule. Jeshi linatakiwa kurudi kambini na vijana hawa wanapaswa kuweka chini silaha".