SUDAN-USALAMA-SIASA

Sudan: Viongozi wa waasi warudi Khartoum, wapokelewa na Waziri Mkuu

Sudan inajaribu kusahau enzi za vita mwezi mmoja baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya serikali na makundi makubwa ya waasi.

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok.
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok. AP / File Photo
Matangazo ya kibiashara

Jumapili hii, viongozi wengine wa makundi ya waasi walirejea nchini na kupokelewa na Waziri Mkuu.

Maelfu ya raia walikusanyika katikati mwa mji wa Khartoum kushangilia kurudi kwa viongozi hawa waasi. Umati wa watu wakiwa na furaha walionekana wakiimba kusherehekea makubaliano ya amani.

"Tulikuwa tunatarajia siku hii," Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alisema wakati akisalimiana na viongozi wa makundi haya ya waasi.

Baadhi wamesema, ziara hii ni ya kwanza jijini Khartoum kwa karibu miaka 20. "Kuanzia leo tutakuwa sehemu ya serikali ya mpito," alisema al-Hadi Idris, kiongozi wa Chama cha Mapinduzi cha Sudan, muungano wa makundi ya waasi.

"Tumekuja kutimiza makubaliano ya amani," alisema Minni Minnawi, mkuu wa tawili lingine la kundi la Ukombozi wa Sudan.Viongozi wa waasi pia walikutana na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Baraza Kuu, ambalo ndilo chombo cha juu zaidi kinachohusika kusimamia mabadiliko hayo.

Kurudi kwa viongozi hawa waasi kunaonekana kama hatua muhimu ya kwanza katika utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwezi uliopita. Vyama tofauti sasa vitalazimika kushughulikia uundaji wa serikali mpya na Baraza kuu mpya ambalo litajumuisha viongozi hawa waasi.