ETHIOPIA-USALAMA

Jeshi la Ethiopia laelekea mji mkuu wa jimbo la Tigray

Vikosi vya Ethiopia vimesonga mbele leo Jumatano kuelekea Mekele, mji mkuu wa jimbo la Tigray, licha ya wito wa kimataifa wa mazungumzo kati ya Addis Ababa na mamlaka katika eneo hili linalotaka kujitenga ili kumaliza mzozo ambao unadumu sasa wiki mbili.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Desemba 7, 2019.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Desemba 7, 2019. © Tiksa Negeri / REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Novemba 4, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitoa agizo kwa jeshi kuingilia kati katika jimbo hili la Kaskazini mwa nchi ambalo lina zaidi ya wakaazi milioni tano, kurejesha utawala wa sheria, baada ya vikosi vya jimbo jilo kuhusishwa katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi la serikali.

Takriban wakimbizi 30,000 wamevuka mpaka na kuingia nchini Sudan. Kulingana na shirika la habari la REUTERS, baadhi yao wamesema kuwa walikuwa wakilengwa na wanamgambo kutoka jimbo jirani la Amhara kwa sababu ni kutoka kabila la Tigray, huku wakidai kuwa mashambulizi ya anga yaliua raia wengi, madai ambayo Addis Ababa inakanusha.

"Serikali ya shirikisho (...) inakanusha kwamba operesheni hii ina upendeleo wowote wa kikabila," kitengo cha serikali kinachosimamia hali hiyo kimesema katika taarifa leo Jumatano.

Watigray, ambao wanawakilisha 5% ya wananchi wa Ethiopia walitawala siasa za nhi hiyo kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 2018.