ETHIOPIA-USALAMA

Mgogoro nchini Ethiopia: Utawala waendelea kuvishtumu vikosi vya Tigray

Wakimbizi wa Ethiopia waliokimbilia karika mji wa Qardarif, Sudan.
Wakimbizi wa Ethiopia waliokimbilia karika mji wa Qardarif, Sudan. AP Photo/Marwan Ali

Majeshi ya serikali kuu ya Addis Abbaba yanaendelea na operesheni yao dhidi ya vikosi vya TPLF, katika jimbo la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed, operesheni hiyo imeingia, , katika hatua yake ya mwisho. Wakati huo huo, mamlaka ya shirikisho nchini humo imeendelea na operesheni yake ya kuwakamata watu wanaoshtumiwa kushirikiana na vikosi vya TPLF kwa kuhatarisha usalama na kutaka kuanzisha uasi dhidi ya serikali kuu ya Addis Ababa.

Wengi wanashutumu utawala kwa ukandamizaji wa kikabila dhidi ya jamii ya Tigray. Hata hivyo Addis Ababa imekanusha.

Wakati huo huo polisi ya Ethiopia imeendelea kuwashikilia watu kadhaa kwa tuhuma mbalimbali. Mamlaka inasema inawashikilia watu 287 wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray .

Hayo yanajiri wakati serikali ya shirikisho imetoa hati ya kukamatwa dhidi ya wanajeshi 76. Maafisa hawa wa ngazi za juu katika jeshi, ikiwa ni pamoja na majenerali, makanali na maafisa wengine, ambao baadhi inasemekana wamestaafu, wanatuhumiwa "kula njama na vikosi vya TPLF kwa kufanya uhaini".

Miongoni mwao, Kanali Gebregziabher Alemseged, ambaye aliongoza wanajeshi wa Ethiopia wakati waliingia Somalia mnamo mwaka 2006. Alibadilishwa miaka miwili baadaye wakati alishtakiwa kwa mauaji.

Maafisa hawa inasemekana walihusika katika shambulio dhidi ya kambi ya vikosi vya shirikisho, hali ambayo ilisababisha kuzuka kwa mzozo mapema mwezi Novemba.

Wakati huo huo Mkuu wa majeshi ya Ethiopia amemshutumu Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani, WHO, kwa kufanya ushawishi kwa maslahi ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), kinachopambana na majeshi ya serikali.

Mamia wameuawa katika mzozo jimboni Tigray tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba.

Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus anatoka katika jamii ya Watigray na alikuwa waziri wa afya katika serikali iliyopita ya Ethiopia,iliyoongozwa na TPLF.