BURKINA FASO-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Burkina Faso inafanya Uchaguzi Mkuu

Masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa Novemba 22 yakitarajiwa kupelekwa katika vituo vya kupigia kura, Burkina Faso, Novemba 21, 2020.
Masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa Novemba 22 yakitarajiwa kupelekwa katika vituo vya kupigia kura, Burkina Faso, Novemba 21, 2020. © Paulina Zidi/RFI

Wananchi wa Burkina faso wanapiga kura leo Jumapili kumchaguwa rais wao mpya na wabunge. Tayari vituo vya kupigia kura vimefunguliwa na zoezi la kupiga kura linaanza kwa wakati wowote.

Matangazo ya kibiashara

Wagombea 13, ikiwa ni pamoja na rais anayemaliza muda wake Roch Marc Christina Kabore na mwanamke mmoja watashiriki katika kinyang'anyiro hicho cha urais.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameipongeza serikali, viongozi wa kisiasa na raia wa Burkina Faso kwa kudumisha mazingira ya kuheshimiana katika wakati wote wa mchakato wa uchaguzi licha ya changamoto lukuki zinazolikabili taifa hilo la Afrika Magharibi.

Katika ujumbe uliotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani, Antonio Guterres ametoa wito kwa wadau wote katika uchaguzi huo kuendeleza mazingira hayo na kuhakikisha kwamba uchaguzi wa kesho Jumapili unafanyika kwa njia ya amani, jumuishi na wa kuaminika.

Katibu Mkuu pia amevitaka vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kufanya kila juhudi kuwalinda raia nchi nzima wakati wakipiga kura kutekeleza haki yao ya demokrasia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Guterres amerejea kusisitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia juhudi za kitaifa za kuwa na utawala wa kidemokrasia, kuchagiza muungano wa kijamii na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu nchini Burkina Faso.

Rais wa sasa aliyeko madarakani Roch Marc Christina Kabore anashiriki uchaguzi huo akisaka muhula wa pili wa miaka 5 huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Eddie Komboigo kiongozi wa chama cha upinzani cha Congress for Democracy and Progress (CDP) chama kilichokuwa cha rais wa zamani wan chi hiyo Blaise Compaore ambaye alitolewa madarakani na machafuko mashuhuri yaliyozuka nchini humo mwaka 2014.

Burkina Faso ina karibu watu milioni moja, wakimbizi wa ndani, waliolazimika kuyahama makaazi yao kufuatia mashambulio yanayotekelezwa na makundi ya yakijihadi.