SENEGAL-MACKY SALL

Senegal: Macky Sall aonya juu ya uwezekano wa kutokea mlipuko wa pili wa COVID-19

Rais wa Senegal, Macky Sall, hapa akiwa jijini Paris, Ufaransa. 27 Agosti 2020.
Rais wa Senegal, Macky Sall, hapa akiwa jijini Paris, Ufaransa. 27 Agosti 2020. ERIC PIERMONT / AFP

Rais wa Senegal Macky Sall amesema ana wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokea wimbi la pili la ugonjwa hatari wa COVID-19, ambalo "litaathiri pakubwa uchumi wa nchi".

Matangazo ya kibiashara

Ijapokuwa Senegal imerekodi idadi ndogo ya vifo ikilinganishwa na nchi zingine duniani na matokeo "ya kuthaminiwa", rais Macky Sall amewataka wananchi wake waendelee kuheshimu zaidi makataa yaliyowekwa dhidi ya kusambaa kwa virusi vya Corona nchini Senegal.

 

"Bado kabisa hatujashinda vita," ameonya rais Macky Sall katika hotuba yake siku ya Alhamisi, Novemba 26.

 

Katika siku za hivi karibuni, kulishuhudiwa ongezeko la idadi ndogo ya visa vipya vya maambukizi nchini Senegal, ambapo visa 20 hadi 30 vilithibitishwa kwa siku, dhidi ya kumi katika wiki chache zilizopita.

 

Wasiwasi hasa unatokana na kesi zinazoripotiwa katika jamii mbalimbali nchini Senegal. "Hii inamaanisha kuwa virusi vinaripotiwa kati ya raia wasioheshimu makataa yaliyowekwa na hao ndio husambaza virusi vya Corona," rais Macky Sall amebaini.

 

Macky Sall amesisitiza juu ya kuheshimu masharti yaliyowekwa, wakati uvaaji wa barakoa na baadhi ya hatua dhidi ya Corona hazitekelezwi.

 

Hata hivyo, Waziri wa Afya, Abdoulaye Diouf Sarr, katika mkutano na waandishi wa habari amehakikisha kwamba hakuna dalili zinazoonyesha kutokea kwa mlipuko mpya wa COVID-19 kwa wakati huu.

 

Wakati huo huo amewataka raia kuwa makini, akibaini kwamba yote yanawezekana. Kulingana na mamlaka ya Afya na takwimu zilizokusanywa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Johns Hopkins, COVID-19 imeathiri karibu watu 16,000 na kuua watu 332 nchini Senegal.