SUDAN KUSINI

Kambi ya Machar yashutumu jeshi la Kiir kuanzisha mapigano Sudani Kusini

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir (kushoto) akiwa na makamu wake wa rais, Riek Machar, mjini Juba, tarehe 20 Feb 2020
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir (kushoto) akiwa na makamu wake wa rais, Riek Machar, mjini Juba, tarehe 20 Feb 2020 REUTERS/Jok Solomun

Mapigano mapya yamezuka katika jimbo la Equatoria ya Kati, Kusini Magharibi mwa jiji kuu Juba, kati ya vikosi vya rais Salva Kiir na Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar.

Matangazo ya kibiashara

Jenerali William Gatjiath Deng, ambaye ni msemaji rasmi wa kijeshi wa Riek Machar, anawashutumu wanajeshi tiifu kwa rais Salva Kiir kuanzisha mapigano hayo ambayo yameingia siku yake ya tatu.

 

Wanajeshi wa SPLAIO, wa Riek Machar, wameshambuliwa na wanajeshi wa SPDF wanaomtii rais Salva Kiir. Wanajeshi wa SPLAIO, walijibu mashambulizi kwa ujasiri na kuwasambaratisha wanajeshi wa kiir walioingia msituni, kulingana na kauli ya Jenerali William Gatjiath Deng.

 

Wakati huo huo msemaji wa rais Salva Kiir, Wek Ateny Wek, amefutilia mbali madai hayo akisema kuwa ni madai yasio kuwa na msingi .

 

Matamshi ya Deng, ni uwongo mtupu. Hakuna kitu kama hicho. Anayoongea Deng ni hadithi ya kubuni. Hakuna mapigano anavyodai. Daktari Riek ni mmoja wa washiriki katika serikali ya mpito, “ amesema Wek Ateny Wek.

 

Aidha Ateny Wek, ametupilia mbali uwezekano wa kutokea mapigano mapya kama yale ya mwaka 2013, ambayo yalisababisha kuvunjika kwa Serikali ya umoja.

 

Hapana. Wanajeshi wa Riek machar, kamwe hawawezi kusababisha mapigano makubwa. Siwezi kusema kutazuka mapigano makubwa tena, “ Wek Ateny Wek ameongeza.

 

Matukio haya yanaripotiwa ni miezi takribani tisa kupita tangu viongozi hawa wawili wakubaliane kuunda serikali ya pamoja.