CHAD

Rais wa Chad, Idriss Déby atimiza miaka 30 madarakani

Rais wa Chad, Idris Deby, wakati mmoja aliongoza vita dhidi ya kundi la kijihadi la Boko Haram
Rais wa Chad, Idris Deby, wakati mmoja aliongoza vita dhidi ya kundi la kijihadi la Boko Haram wotzup.ng

Desemba 1, 1990, Idriss Déby alichukua hatamu ya uongozi wa nchi ya Chad kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa, Hissène Habré.

Matangazo ya kibiashara

Ni miaka miaka 30 tangu Idriss Déby, achukue madaraka kabla ya kupewa cheo cha marshal mwanzoni mwa mwaka huu.

 

Licha ya maandamano ya kisiasa, utawala wake unaonekana kuwa imara.

 

Miaka 30 iliyopita, Desemba 1, 1990, akiwa kiongozi wa kundi la wapiganaji la Wokovu wa Uzalendo, MPS, Idriss Déby aliuteka mji wa Ndjamena, mji mkuu wa Chad alioukimbia mtangulizi wake Hissène Habré ambaye vikosi vyake vilishindwa kuhimili mashambilizi ya vikosi vya MPS.

 

Desemba 4 Idriss Débyaliteuliwa kuwa rais wa Baraza la taifa, wakati Hissène Habré akikimbilia Senegal.

 

Miezi ishirini mapema, mnamo Aprili 1, 1989, Idriss Déby na washirika wake wachache ambao walitafautiana na kiongozi wao Hissène Habré walijaribu kufanya mapinduzi.

 

Watu hao walioshirikiana na Idriss Déby, ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Mahamat Brahim Itno, na Hassan Djamouss, Amiri Jeshi Mkuu wa jeshi la Chad.

 

Lakini mpango wao wa mapinduzi ulitibuliwa, washirika wake watatu na askari kadhaa walijaribu kuondoka Chad kuelekea Sudan.

 

Djamouss na Itno walikamatwa na kuuawa na vyombo vya usalama vya Hissène Habré.

 

Kutoka Sudan, Kanali Idriss Déby alifanikiwa kushirikiana na makundi mbalimbali ya upinzani dhidi ya Hissène Habré na mnamo Machi 11, 1990 aliunda kundi la wapiganaji la MPS katika eneo la Bamina nchini Sudan.

 

Ufaransa yajitenga na Habré

 

Wakati huo huo, uhusiano kati ya Hissène Habré na Ufaransa ulivunjika. Rais wa Chad Hissène Habré wakati huo alikataa kutii agizo la mwenzake wa Ufaransa François Mitterrand, ambaye aliomba katika hotuba yake katika mkutano wa Ufaransa na Afrika huko La Baule mnamo 1989 kwamba serikali madarakani barani Afrika zinatakiwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi na demokrasia ikiwa zinataka kuendelea kuungwa mkono na Ufaransa.

 

Habré, ambaye aliamua kupinga mamlaka ya zamani ya kikoloni, alipingana na kauli hiyo kwa kuandaa uchaguzi wake kwa muhula wa miaka saba mwezi Desemba 1989. Uchaguzi wa wabunge uliruhusu kuanzishwa kwa Bunge ambalo halikuridhishwa na mfumo wake wa kidemokrasia.

 

Kulingana na baadhi ya wachambuzi, nia ya rais wa Chad kutumia mafuta ya Chad kwa gharama zote akiungwa mkono na Marekani ambapo alikuwa mmoja wa washirika wakuu katika vita dhidi ya Muammar Gaddafi wa Libya, ni mpoja ya sababu ya kuanguka kwa utawala wake.