LIBYA

Umoja wa Mataifa watia wasiwasi na kuendelea kuingizwa kwa silaha nchini Libya

Mapigano yameendelea kushuhudiwa nchini Libya, umoja wa Mataifa ukieleza hofu yake kuhusu kuingizwa kwa silaha
Mapigano yameendelea kushuhudiwa nchini Libya, umoja wa Mataifa ukieleza hofu yake kuhusu kuingizwa kwa silaha Getty Images

Libya bado ina wanajeshi elfu 20 kutoka nchi za kigeni pamoja na mamluki, licha ya kuwepo kwa mkataba wa maelewano uliotiwa saini mwezi Oktoba, kuzuia uingizwaji wa silaha na vikosi vya kigeni nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Stephanie Williams, amekiri kushangazwa na hali hiyo ambayo ameitaja kuwa ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa nchi ya Libya.

Aidha, amesema kuna kambi kumi za kijeshi nchini humo, ambazo zinatumiwa na wanajeshi hao wa kigeni na mamluki, hali anayosema inatoa nafasi ya silaha zaidi kuingizwa.

Mwezi Oktoba, wanajeshi wa serikali ya umoja wa kitaifa(GNA) inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na wale wanaongozwa na mpinzani wa serikali ya TripoliJjenerali Khalifa Haftar walisaini mkataba, uliotaka wanajeshi na wapiganaji wote wa kigeni kuondoka nchini Libya ndani ya siku tisini.

Mwezi Novemba, pande zinazohasimiana nchini Libya zilikubaliana kuwa nchi hiyo iwe na Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba mwaka 2021 lakini wakashindwa kukubaliana ni nani ataongoza katika kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi huo.