ETHIOPIA

Ethiopia: Waasi wadai kuwepo na maandamano katika mji mkuu wa Tigray

Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. AFP/Monirul BHUIYAN

Kiongozi wa waasi wa Tigray Debretsion Gebremichael amedai kuepo na maandamano huko Mekele, mji mkuu wa jimbo la Tigray uliochukuliwa na vikosi vya serikali mwishoni mwa juma lililopita kutoka mikononi mwa waasi.

Matangazo ya kibiashara

Jimbo la Tigray limekuwa likikumbwa na hali ya sintofahamu baada ya mapigano yaliyodumu mwezi mmoja.

 

Hata hivyo, picha zilizorushwa kwenye runinga ya umma huko Mekele inaonyesha watu wakifanya mazoezi huku wengine wakikaa kwenye viti. Kaimu mkuu wa jimbo la Tigray, Mulu Nega, aliyeteuliwa na serikali kuu ya Addis Ababa, kwa upande wake, ametangaza kwamba amani imerejea katika jimbo hilo.

 

Vikosi vya Tigray People's Liberation Front (TPLF) viliingia vitani mnamo Novemba 4 dhidi ya serikali ya shirikisho huko Addis Ababa, ambayo iliamuru jeshi kuingilia kati katika jimbo hili la Kaskazini mwa nchi ili kurejesha utawala wa sheria, baada ya kulaumu vikosi vya TPLF kuhusika na shambulio dhidi ya kambi ya wanajeshi wake.

 

Ni ngumu kudhibitisha madai ya kambi moja au nyingine kwani upatikanaji wote wa simu na wavuti kwa mkoa huo umekatwa. Hata hivyo, inakadiriwa kuwa mapigano hayo yamewaacha maelfu wamekufa na kusukuma zaidi ya watu 45,000 kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Sudan.

 

Hata hivyo ni vigumu kuthibitisha kile kinachodaiwa na kila upande, kwa mawasiliano katika jimbo la Tigray yamekatwa.

 

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umeitaka Ethiopia kurudisha mawasiliano Tigray.

 

Jumatano Ethiopia ilitangaza rasmi kwamba inaruhusu Umoja wa Mataifa kupeleka msaada Tigray kwa mujibu wa makubaliano yaliyoonekana na shirika la habari la AFP.

 

Na kwenye makubaliano hayo imeelezwa wazi kwamba Umoja wa Mataifa na washirika wake katika masuala ya kiutu wanaweza kuwapelekea msaada raia kwenye maeneo yanayodhibitiwa na serikali ndani ya jimbo hilo la Tigray. Ingawa leo Ijumaa Umoja huo wa Mataifa umelalamika kwamba vita vinaendelea na juhudi za kupeleka msaada zinatatizwa.