ETHIOPIA-TIGRAY

Mapigano yakwamisha upelekwaji wa misaada kwenye eneo la Tigray

Wapiganaji wa eneo la Tigray nchini Ethiopia
Wapiganaji wa eneo la Tigray nchini Ethiopia France24

Umoja wa Mataifa unasema, mapigano yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ya mji wa Tigray nchini Ethiopia, hali inayokwamisha shughuli za upelekaji wa misaada ya kibinadamu.

Matangazo ya kibiashara

Haya yanajiri wakati huu ripoti zikionesha kuwa mamilioni ya watu wanaelekea kukosa chakula.

Maofisa wa umoja wa Mataifa wameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hawakuweza kufikisha misaada kama walivyokubaliana na utawala wa Addis Ababa, hasa kwenye maeneo ambayo yanakaliwa na vikosi vya Serikali.

Jeshi liliingia kwenye mji wa Mekele mwishoni mwa juma lililopita na kutangaza kumalizika rasmi kwa operesheni za kijeshi kwenye mji wa Tigray.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa katika mji wa Tigray, huku maelfu wengine wakikimbilia nchi jirani ya Sudan kuomba hifadhi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa, vimeripoti kuhusu uwepo wa mapigano kwenye baadhi ya maeneo licha ya kuwa Serikali inakanusha kuhusu kuendelea kwa mapigano.

Viongozo wa TPLF ambao wanaongoza eneo la Tigray, licha ya kukimbia mji huo, wameapa kuendelea na vita kwa kile walichosema hawawezi kuona mji wao unachukuliwa na wavamizi.