DRC

Rais Tshisekedi kuchukua maamuzi kuhusu mvutano wa kisiasa kati ya FCC na CASH

Rais wa DRC, Félix Tshisekedi
Rais wa DRC, Félix Tshisekedi Sumy Sadurni / AFP

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Thisekedi, siku ya Jumapili anatarajiwa kutangaza maamuzi kuhusu mvutano wa kisiasa ambao umekuwa ukishuhudiwa kati ya muungano wake wa CACH na ule wa FCC wa rais wa zamani Joseph Kabila, walioungana miaka iliyopita kuunda serikali ya pamoja.

Matangazo ya kibiashara

Hotuba ya rais huyo imethibitishwa na msemaji wake, Kasongo Mwema, kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Wachambuzi wa siasa nchini DRC wanasema kuwa rais Tshisekedi ameshindwa kutekeleza kikamilifu mageuzi kwa sababu hana udhibiti wa Bunge na huenda anakwamishwa na wabunge wanaomuunga mkono rais wa zamani.

Kumekuwa na madai kuwa rais Tshisekedi anataka kuvunja ushirikiano na FCC, muungano alioingia nao kwa makubaliano miaka miwili iliyopita na kuunda serikali.

Muungano wa FCC unaituhumu ule wa CACH unaoongozwa na rais Thsisekedi kuwa na mpango wa kuwahonga wabunge wa muungano wa FCC ili kumaliza nguvu yake katika Bunge la kitaifa ili kulidhibiti.

Ripoti zinasema kuwa hali imekuwa kwa muda wa siku tatu zilizopita, na sasa uongozi wa Bunge ukiongozwa na spika wa Bunge Jeannine Mabunda, umetoa wito kwa Baraza lenye wazee wenye busara kuchunguza madai hayo.

Baadhi ya wabunge wa FCC wanadaiwa kuwa wamepokea kati ya Dola Elfu Saba hadi Elfu Tisa na tayari wameungana na upande wa rais Tshisekedi.

Hata hivyo, uongozi wa CACH unapinga madai ya kuwahonga wabunge wa FCC na kusema, wale wanaoamua kujiunga na upande wao, wanafanya hivyo kwa hiari yao.