GHANA-SIASA-UCHAGUZI

Raia wa Ghana wanapiga kura kumchagua rais na wabunge

Wagombea wakuu wa urais nchini Ghana Nana Akufo-Ado na John Mahama wa chama cha NDC
Wagombea wakuu wa urais nchini Ghana Nana Akufo-Ado na John Mahama wa chama cha NDC RFI

Wananchi wa Ghana hivi leo wanapiga kura kumchagua rais na wabunge, uchaguzi ambao unafanyika katika kipindi cha janga la Corona, ambapo watu zaidi ya Elfu Hamsini wameripotiwa kuambukizwa nchini humo na watu wasiopungua mia tatu wamefariki kutokana na virusi hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Ni uchaguzi ambao unafanyika kukiwa na matumaini ya kutokuwa na vurugu kufuatia sheria iliopitishwa mwaka uliopita ya kupiga marufuku makundi ya vijana yanayokusanywa na wanasiasa ili kulinda kura zao, na kupendekeza kifungo cha hadi miaka kumi jela.

Wagombea wakuu katika uchaguzi huo, rais wa sasa Nana Akufo Ado wa chama cha New Patriotic Party (NPP) na mpinzani wake wa muda mrefu, rais wa zamani John Mahama, wa chama cha National Democratic Congress (NDC) watakuwa wakipambana kwa mara ya tatu.

Ukosefu wa ajira, usalama na athari za janga la Corona ni baadhi tu ya mambo ambayo raia wa Ghana watazingatia wakati wakipiga kura.

Jumla ya wagombea 11 miongoni mwao wanawake watatu watapambana katika uchaguzi huo, ushindani mkali ukitarajiwa kati ya rais wa sasa Nana Akufo-Ado na rais wa zamani John Mahama wa chama cha National Democratic Congress (NDC).